1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aomba silaha na idhini ya kuzitumia kuipiga Urusi

6 Septemba 2024

Viongozi wa kundi la nchi za Magharibi, washirika wa Ukraine waahidi kuipatia msaada zaidi Ukraine katika vita vyake na Urusi.

https://p.dw.com/p/4kNM2
Waziri wa ulinzi wa Marekani  Lloyd Austin na rais Volodymyr Zelensky
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na rais Volodymyr ZelenskyPicha: Heiko Becker/REUTERS

Washirika wa Ukraine wa nchi za Magharibi wanaokutana katika kambi ya kijeshi ya Marekani hapa Ujerumani,wameahidi kuisadia nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya Urusi. 

Jioni hii rais Zelensky amefanya mazungumzo na Kansela Olaf Scholz yaliyogusia suala juu ya mkutano wa pili wa kilele wa amani kuhusu Ukraine.

Mazungumzo yao yamefanyika mjini Frankfurt ambako pia Zelensky alihudhuria mkutano wa washirika wa Magharibi wa nchi yake ukilenga kuipatia msaada wa silaha. Mkutano huo umefanyika kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ramstein ukiongozwa na waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin.

Viongozi wa kundi la washirika wa Ukraine-Ramstein
Washirika wa Ukraine katika mkutano wa RamsteinPicha: Michael Probst/AP/picture alliance

Kwenye mkutano huo Zelensky  amewahimiza washirika wake wa kundi la nchi 50 wanaotaka kuisadia Ukraine kutowa msaada zaidi wa silaha ikiwemo makombora ya masafa marefu na ndege za kivita.

"Tunahitaji kuwa na makombora yenye uwezo mkubwa wa kushambulia masafa marefu sio tu kuyatumia katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa kwa mabavu  lakini pia tutakayoweza kuyatumia kushambulia ndani ya maeneo ya Urusi na kuilazimisha Urusi ifuate mkondo wa kutafuta amani.''

Kiongozi huyo wa Ukraine amesisitiza kwamba wanahitaji kuitia adabu Urusi na kuifanya miji ya nchi hiyo na hata wanajeshi wake kutafakari ikiwa wanahitaji amani au wanamuhitaji Putin.

Ahadi za mataifa ya Magharibi kwa Ukraine.

Tangu mwaka 2022 nchi wanachama wa kundi la washirika wa Magharibi wanaounga mkono harakati za Ukraine dhidi ya Urusi wameshatowa kiasi ya billioni 106 za kuisaidia nchi hiyo kujilinda,ambapo Marekani peke yake imetowa zaidi ya dola bilioni 56 kwa ujumla.Soma Pia: Ukraine yatarajia maamuzi mazito kutoka Ramstein

Na kwenye mkutano huu wa Ramstein waziri wa ulinzi wa Marekani anayeongoza mkutano huo,Lloyd Austin amesema Washington itatowa msaada mwingine wa silaha kwa Ukraine wa dola milioni 250 utakaojumuisha mifumo ya ulinzi wa anga pamoja na makombora.

Waziri wa ulinzi-Boris Pistorius
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani-Boris PistoriusPicha: Uwe Anspach/dpa/picture alliance

Ujerumani kwa upande wake,waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Boris Pistorius amesema ahadi waliyoitowa ya kutuma mifumo ya ulinzi na hasa hasa mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot itapelekwa Ukraine katika kipindi cha msimu wa baridi, ili kuisadia nchi hiyo kulinda miundo mbinu yake. 

"Maana yake ni kwamba tutaendelea na mchakato wa kuisadia Ukraine. Na juu ya hilo nataka kutangaza kwa mara ya kwanza leo taarifa hizi mpya. Tutaipatia Ukraine vifaru vya kijeshi vya kisasa 12,ambapo sita vitawasili mwaka huu na vingine sita vitapelekwa mwakani.Vyote thamani yake ni yuro milioni 150.''

Waziri wa ulinzi wa Canada Bill Blair amesema ameshawishika na kilichozungumzwa na rais Zelensky kuhusu kutaka ridhaa ya kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi,akisema anamuunga mkono kiongozi huyo na kwamba anataraji viongozi wengine wa nchi za Magharibi wataiunga mkono fikra hiyo ya Zelensky.Soma Pia: Marekani na Ujerumani kujadili misaada kwa Ukraine

 Boris Pistorius na  Rustem Umjerow
Mawaziri wa ulinzi wa Ujerumani na UkrainePicha: Uwe Anspach/dpa/picture alliance

Mkutano huu umekuja katika wakati ambapo yameshuhudiwa matukio kadhaa katika mapambano ya Ukraine dhidi ya Urusi,wakati Ukraine ikiendesha operesheni yake ya kwanza ya kuishambulia Urusi huku pia ikikabiliwa na kitisho kikubwa kutoka kwa wanajeshi wa Urusi kwenye eneo lake muhimu la Donbas.

Ukraine inavyozizatiti kuishambulia Urusi.

Mpaka sasa mashambulizi ya kushtukiza ya Ukraine ndani ya ardhi ya Urusi kwenye eneo la Kursk yamefanikiwa kuifanya Ukraine kunyakuwa eneo la kilomita 1,300 la Urusi na kuuwa au kuwajeruhi takriban wanajeshi 6000 wa Urusi kwa mujibu wa rais Zelensky.

Hivi leo Urusi imefyetuwa makombora matano katika mji wa Pavlohrad ulioko kwenye mkoa wa mashariki wa Dnipropetrovsk, na kusababisha kiasi watu 50 kujeruhiwa

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW