1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy: Hadi wanajeshi 3,000 wa Ukraine wauwawa vitani

16 Aprili 2022

Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema kati ya wanajeshi 2,500 na 3,000 wa Ukraine wamekufa hadi sasa katika vita vya taifa hilo na Urusi na kwamba wengine 10,000 wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4A12Z
Russland Ukraine Konflikt I  Dnipro, Dnipropetrovsk
Rais Zelenskiy amesema hadi wanajeshi 3,000 wa Ukraine wamekufa tangu Urusi iivamie UkrainePicha: Celestino Arce Lavin/ZUMA/picture alliance

Hayo ameyasema jana wakati alipozungumza na televisheni ya CNN ya Marekani katika kipindi hiki ambacho vita vya Urusi na Ukraine vikipindukia siku 50. Katika mahojiano yake hayo ambayo kwa upana yalirushwa moja kwa moja jana Ijumaa Zelensky amesema wanajeshi wengine wa Ukraine takribani 10,000 wamejeruhiwa na ni vigumu kujua wangapi miongoni mwa hao watapona.

Zelensky amelinganisha idadi hiyo na ile ya Urusi inayoonesha wanajeshi wa Ukraine kati ya 19,000 na 20,000 wameuwawa katika vita hivyo. Mataifa ya Magharibi yanakadiriwa maelfu ya wanajeshi pia wameuwawa kwa upande wa Urusi.

Lakini serikali ya Urusi hivi karibuni ilitangaza kuwa wanajeshi wake kiasi ya 1,350 wameuwawa katika vita hivyo tangu vianze.

Zaidi ya watu 2,800 wamefanikiwa kuokolewa katika maeneo ya vita.

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine | Mariupol
Sehemu ya mji wa bandari wa MariupolPicha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali nchini Ukraine  zaidi ya raia 2,800 wamefanikiwa kuokolewa katika baadhi ya miji yenye makabiliano makali huko mashariki mwa Ukraine. Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk ameandika katika ukurasa wake wa telegram kwamba kiasi ya wakimbizi 2,500 waliwasili jana Ijumaa katika mji wa kusini wa Zaporizhzhya, wakiwemo 363 kutoka katika eneo lililovurugwa vibaya kwa vita la Mariupol.

Awali, ofisi ya mwendesha mashtaka ya Kharkiv ilitoa taarifa inayosema raia saba wameuwawa na wanajeshi wa Urusi wakati wakijaribu kupita njia salama kwa kutumia usafiri wa basi, kukimbia katika kijiji chenye machafuko cha Borova. Na wengine 27 wameripotiwa kujeruhuwa katika shambulizi hilo.

Hakuna msaada wa kiutu unaoruhisiwa kuingia Mariupol hadi sasa.

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine | Zerstörung in der Region Mariupol
Hali ngumu ya wakazi wa mji wa MariupolPicha: Sergei Bobylev/TASS/picture alliance

Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, David Beasley amesema hakuna msafara wowote wa msaada wa kiutu ambao umeruhusiwa kuingia katika eneo la Mariupol tangu mji huo wa bandari uzingirwe na majeshi ya Urusi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili kwake nchini Ukraine kiongozi huyo aliongeza kwa kusema inaaminika kuwa idadi ya watu takribani laki moja bado ipo katika mji huo, lakini upatikanaji wa maji na chakula unaweza kwisha wakati wowote.

Mapigano bado yanaendelea katika miji ya Popasna na Rubizhne.

Kwengineko nchini Ukraine, vikosi vya Urusi vinaendelea kuvurumisha makombora yake katika miji ya Popasna na Rubizhne huko katika jimbo la Luhansk mashariki mwa Ukraine. Jeshi la Ukraine limesema watu 7 pia wameuwawa kwa makombora mjini Kharkiv hukohuko mashariki. Katika eneo hilo pia ofisi ya mwendesha mashtaka imesema watu 35 wameripotiwa kujeruhiwa.

Huko nyuma mwaka 2014 Urusi iliwaunga mkono na wanaotaka kujitenga kwa kuanzisha mapigano katika miji ya Donetskna Luhansk. Lakini kwa sasa inashiriki moja kwa moja. Ukraine inasema katika kipindi cha masaa 24 imeweza kuviteketeza vifaru kadhaa vya Urusi na mizinga .

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya raia wa Ukraine milioni 4.7 wamelikimbia taifa hilo tangu kuanza kwa vita mwishoni mwa Februari, ambapo wengine wamesalia kuwa wakimbizi wa ndani wa taifa hilo kutokana na mgogoro huo.

Chanzo: DPA