1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelenskiy asema usitishaji mapigano utainufaisha tu Urusi

12 Januari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema usitishaji mapigano katika vita na Urusi hautapelekea majadiliano ya kisiasa na utainufaisha tu Urusi kwa sababu hilo litairuhusu nchi hiyo kuimarisha ugavi wake wa silaha.

https://p.dw.com/p/4b9am
Tallinn, Estonia | Ziara ya Rais Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiwa katika mazungumzo na Rais wa Estonia Alar Karis mjini Tallinn, Estonia, Januari 11, 2024. Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS/REUTERS

Rais Zelenskiy aliyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Estonia, ambayo ilikuwa sehemu ya ziara pana ya mataifa ya kanda ya Baltiki yakiwemo Lithuania na Latvia, ambayo yanaiunga mkono pakubwa Ukraine katika mzozo wake na Urusi, pamoja na makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami NATO.

''Usimamishaji kwenye uwanja wa vita kwenye ardhi ya Ukraine siyo usimamishaji wa vita. Siyo mwisho wa vita. Haupelekei mazungumzo ya kisiasa na Shirikisho la Urusi au na mtu mwingine," alisema Zelenskiy wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Usimamishaji huu utainufaisha tu Urusi, kwa nini? Kwa sababu tunaelewa kiasi wanachozalisha Urusi leo. Tunajua ni droni ngapi, maroketi mangapi wanazalisha kila siku,'' aliongeza.

Mataifa hayo matatu ya Baltiki ndiyo yalikuwa ya kwanza ya Magharibi kuipatia Ukraine silaha katika wiki za kwanza kabla ya uvamizi wa Urusi Februari 2022.

Soma pia: Urusi yaivurumishia mvua ya makombora Ukraine

Zelenskiy alisema Urusi ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa risasi na inapambana kujenga upya kikosi chake maalumu, ambacho kilikuwa kinashawishi utendaji katika uwanja wa vita.

Latvia | Volodymyr Zelenskiy mjini Riga
Rais wa Latvia Edgars Rinkevics (kulia), na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy (kushoto) wakishikana mikono baada ya mkutano wao wa pamoja wa habari mjini Riga, Latvia, Alhamisi Januari 11, 2024. Picha: Roman Koksarov/AP Photo/picture alliance

Amedai kuwa Urusi ilikuwa inajadili ununuzi wa makomboroa kutoka Iran na kwamba vikosi vya Urusi vimepokea zaidi ya risasi milioni moja kutoka Korea Kaskazini.

Miito ya kuanza mazungumzo na Urusi

Zelenskiy amekataa kuzungumzia matamshi yaliotolewa na waziri wa ulinzi wa Italia Guido Crosetto siku ya Jumatano, kwamba muda umewadia wa kuipa nafasi diplomasia katika mzozo huo.

Waziri Crosetto aliliambia bunge la Italia kwamba mashambulizi ya kujibu ya Ukraine hayakutoa matokeo yaliotarajiwa, na kwamba hali y akijeshi imetazamwa kwa uhalisia.

Alisema kwa mtazamo huo, inaoenekana kwamba wakati umefika wa kufanya diplomasia, sambamba na kuendeleza msaada wa kijeshi, kwa sababu kuna visharia kadhaa muhimu kutoka pande zote.

Alisema Urusi inazidi kuonyesha utayari wa kufanya majadiliano na kuulinda uchumi wake, huku msimamo wa Ukraine ukionekana kuelegea kuliko hapo awali.

Soma pia: Zelenskiy asema baridi inafanya mazingira ya mapigano kuwa magumu kwa majeshi yake

"Yote hayo yanapaswa kuzingatiwa katika njia ya kuelekea majadiliano ili kumaliza mzozo huo na mchakato wa kurekebisha uhusiano, siyo tu wa Urusi na Ukraine, bali pia na mataifa ya Magharibi", alisema waziri Crosetto.

Zelenskiy mjini Vilnius, Lithuania
Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda (kati-kulia) na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy (kati kushoto) wakiwasili kwa mazungumzo katika Kasri la Rais mjini Vilnius, Januari 10, 2024.Picha: Petras Malukas/AFP/Getty Images

'Hakuna shinikizo kutoka kwa washirika'

Hata hivyo, Zelenskiy amesema hakukuwa na shinikizo kutoka nchi washirika kwao kuacha kupigana dhidi ya Urusi, mapigano ambayo amekiri kwamba yatakuwa vigumu sana kwa nchi yake bila kupata msaada wa kifedha uliocheleweshwa kutoka Umoja wa Ulaya.

Urusi imesema iko tayari kwa mazungumzo ya amani ikiwaUkraine itazingatia "uhalisia mpya", ikimaanisha kukubali kwamba Urusi inadhibiti karibu asilimia 17 ya ardhi ya Ukraine.

Zelenskiy amekataa wazo lolote kwamba Moscow inataka majadiliano, akisema inaweza kukubali tu hilo ikiwa litaisaidia kupumzika na kuimarisha jeshi lake.

Chanzo: Mashirika