1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR : Uchaguzi wa ushindani mkali wafanyika Z’bar

30 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CENH

Wapiga kura katika visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania wamepiga kura leo katika uchaguzi wenye ushindani mkali wa Rais,wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani huku kukiwa na ulinzi mkali,vurugu za hapa na pale na madai ya udanganyifu.

Kumekuwepo na repoti zinazosema kwamba askari wamefyatuwa mabomu ya kutowa machozi katika mapambano nje ya kituo kimoja cha kupigia kura katika mji mkongwe wa Zanzibar. Wanajeshi walifika katika kituo hicho wakati wafuasi wa upinzani walipochemka kwa hasira kutokana na kuwasili kwa makundi ya wafuasi wa serikali wakiwa kwenye magari yaliokuwa yakichungwa na wanajeshi.

Kwa mujibu wa mashahidi wa shirika la habari la Uingereza Reuters wanajeshi hao waliwafukuza wafuasi wa upinzani ambao walikuwa wakivurumisha mawe na waliwasaidia wafuasi hao wa serikali kujiunga katika msururu nje ya kituo cha kupigia kura.

Rais Amani Abeid Karume amewaambia waandishi wa habari wakati akipiga kura yake katika eneo la Kiembesamaki kwamba anafikiri uchaguzi huo utakuwa wa amani kinyume na vile watu wanavyofikiria.

Mpinzani mkuu wa Karume Seif Sharrif Hamad wa chama cha CUF ambaye alipoteza chaguzi mbili zilizopita ameapa kufanya maandamano makubwa kama yale ya Ukraine iwapo uchaguzi huu wa leo utafanyiwa udanganyifu.

Uchaguzi huo ni mtihani wa sifa ya Tanzania kama kielelezo cha utulivu kwa Afrika.

Uchaguzi huo wa Zanzibar unafanyika kabla ya ule wa Tanzania nzima ambao umeahirishwa hadi mwezi wa Desemba kutokana na kifo cha mgombea mwenza wa chama kimoja cha upinzani.