1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR: Rais Karume ataka utulivu katika mwezi wa Ramadhan

5 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEUy

Rais wa kisiwa chenye utete wa kisiasa cha Zanzibar nchini Tanzania hapo jana ametowa wito wa kuwepo kwa utulivu wakati mwezi wa mtukufu wa mfungo wa Ramadhan ukianza huku kukiwa na kampeni kali za jazba kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwezi huu.

Rais Aman Abeid Karume ambaye anagombania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wenye ushindani mkali wa Oktoba 30 amesema Waislamu wana wajibu wa kuwaheshimu majirani zao,wageni na mahasimu wa kisiasa hususan katika mwezi huu wa Ramadhan.

Katika hotuba yake ya nusu saa kwa njia ya radio na televisheni amesema amani na utengamano lazima vidumishwe katika mwezi huu licha ya ukweli kwamba wako kwenye kipindi cha uchaguzi na ametaka matumizi ya nguvu na lugha za matusi visipewe nafasi wakati huu.

Wito huo wa Karume unakuja baada ya wito kama huo kutolewa na mgombea wa Rais kwa chama cha upinzani cha CUF kisiwani Zanzibar Seif Sharrif Hamad ambaye amekuwa akilalamika vikali juu ya utawala mbaya na unaokwenda kinyume na sheria wa chama tawala cha CCM.