1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR : Polisi wafyatuwa mabomu ya kutowa machozi

31 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEN3

Vikosi vya usalama leo vimetumia mabomu ya kutowa machozi na mizinga maji pamoja na bakora dhidi ya wafuasi wa upinzani huko Zanzibar nchini Tanzania.

Chama cha Wananchi CUF kimesema kwamba wakati zaidi ya theluthi mbili ya kura zikiwa zimehesabiwa imejipatia asilimia 54.2 dhidi ya asilimia 45.7 iliyojipatia serikali ambayo imekuwa madarakani kwa miongo minne katika visiwa vya Zanzibar halikadhalika nchini Tanzania.

Maafisa wa uchaguzi na chama tawala cha CCM hawakuzungumzia matokeo hayo ambayo yanatazamiwa kutangazwa rasmi hapo Jumaatano.

Wafuasi wa CUF waliokuwa wakisheherekea walimiminika katika mitaa ya mji mkongwe kuanzia asubuhi wakiimba na kucheza ngoma lakini hali hiyo inasemekana ilibadilika na kuwa vita vya kufukuzana na polisi na wanajeshi waliofyetuwa mabomu ya kutowa machozi katika vichochoro vya mji huo ambapo vijana waliwakejeli na mara nyengine kuwavurumishia mawe.

Waandishi wa habari wa shirika la habari la Uingereza Reuters wameshuhudia takriban watu 20 wakichukuliwa na magari ya polisi wengine wakipigwa mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa na waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa waliomiminika Zanzibar.

Wakati huo huo kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika Baleka Mbeta amesifu jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika licha ya kuwepo kwa madai ya udanganyifu na vurugu za hapa na pale ambapo kwayo watu saba wamejeruhiwa.

Amesema uchaguzi huo wa jana kwa kiasi fulani ulikuwa wa amani na umeandaliwa vyema lakini hakusema iwapo chombo hicho cha Afrika kinaamini kwamba ulikuwa huru na wa haki.