1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR : Kagame awataka Wazanzibari kudumisha amani

14 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFDu

Rais Paul Kagame wa Rwanda hapo jana ametowa wito wa kuwepo amani katika visiwa vyenye utete wa kisiasa vya Zanzibar nchini Tanzania ambavyo hivi karibuni vilikumbwa na vurugu za kisiasa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa hapo mwezi wa Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais katika mkutano wa faragha na Rais Amani Abeid Karume Kagame amewataka wananchi wa Zanzibar kufanya jitihada kubwa kulifanya eneo lao kuwa la amani kabla ya kufanyika kwa uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika tarehe 30 mwezi wa Oktoba.

Chama tawala nchini Tanzania CCM na chama kikuu cha upinzani CUF vilitia saini makubaliano ya kukomesha uhasama hapo mwaka 2001 baada ya takriban watu 40 kuuwawa hapo mwaka 2000.

Lakini kabla ya uchaguzi huu wa mwezi wa Oktoba vurugu kati ya wafuasi wa vyama hivyo viwili zimeanza tena kupamba moto na mara kwa mara zimetibuwa zoezi la kuandikisha wapiga kura na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali visiwani humo.

Rais Paul Kagame ambaye amewasili nchini Tanzania hapo Alhamisi kwa ziara ya siku tatu pia amemshinikiza Rais Benjamin Mkapa kuliingiza taifa lake la Afrika ya kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inazijumuisha Kenya,Uganda na Tanzania kwa kusema kwamba muungano wa kikanda ni njia pekee ya maendeleo kwa nchi za kimaskini za Afrika.