Watu 3,000 waliokufa kwa mafuriko Libya wamezikwa
13 Septemba 2023Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya upande wa Mashariki nchini Libya Tarek Al Kharraz, amesema watu 1,100 ambao hawakutambuliwa wamezikwa katika makaburi ya watu wengi.
Kwa mujibu wa Tarek, mazishi hayo yamefanyika Jumatano baada ya mengine ya watu 2,090 kufanyika Jumanne, baada ya utambulisho wao kuthibitishwa rasmi.
Maafisa wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka
Hata hivyo, waziri huyo amesema ni vigumu kutoa takwimu rasmi ya vifo vilivyotokana na mafuriko, kwa sababu baadhi ya miili imezikwa na familia zao bila ya kuandikishwa.
Waziri huyo wa mambo ya ndani ya Libya amesema anatarajia idadi ya vifo kuongezeka, kwa sababu takribani watu 9,000 hawajulikani walipo. Tarek amesema idadi ya watu waliokufa kwa mafuriko hayo kwenye mji wa Derna, imefikia 5,200.
Halmashuri Kuu ya Umoja wa Ulaya imetangaza kuwa umoja huo utatoa msaada wa dharura wenye thamani ya euro 500,000 kwa ajili ya Libya. Kamishna anayehusika na usimamizi wa majanga wa Umoja wa Ulaya, Janez Lenarcic, amesema nchi za Ujerumani, Romania na Finland zimetoa mahema, vitanda vya kukunja, mablanketi, majenereta 80, vyakula, mahema ya hospitali na matanki ya maji.
Kwa mujibu wa Lenarcic, msaada huo uko njiani kuelekea kwenye mji wa Derna ambao umehairibiwa vibaya, na umetolewa kutokana na ombi rasmi la kupatiwa msaada ambalo limetolewa na mamlaka nchini Libya Jumanne.
Msaada wa Ufaransa
Ufaransa nayo imepeleka msaada wa kibinadamu nchini Libya baada ya Rais Emmanuel Macron kuzungumza kwa njia ya simu na mkuu wa Baraza la Rais la Libya, Mohammed al-Menfi. Msemaji wa serikali ya Ufaransa, Olivier Veran, amesema nchi hiyo imepeleka timu ya uokozi ya watu wapatao 50, na Rais Macron ametoa salamu zake za pole kwa familia na ndugu wa maelfu ya wahanga.
''Ufaransa pia inatoa msaada wa kifedha kwenye taasisi za Ulaya, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kimataifa ambayo yanawasaidia wananchi wa Libya,'' alieleza Veran.
Huku hayo yakijiri wizara ya Uhamiaji ya Misri imesema kuwa imeipata miili 87 ya raia wake ambao wamekufa kutokana na kimbunga Daniel nchini Libya. Miili hiyo leo imerejeshwa nyumbani na jeshi la Misri na tayari imezikwa kwenye miji yao.
Juhudi za uokozi zaendelea Morocco
Wakati huo huo, juhudi za uokozi zinaendelea nchini Morocco kuwatafuta wahanga wa tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo wiki iliyopita.
Timu ya uokozi ya kikosi cha jeshi la ulinzi wa raia imeendelea kuwapeleka majeruhi katika hospitali mjini Marrakesh na kutoa misaada ya msingi, ikiwemo chakula na mablanketi kwenye miji kadhaa.
Zaidi ya watu 2,900 wamekufa kutokana na tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter na wengine 5,530 wamejeruhiwa. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 300,000 wameathirika kwenye mji wa Marrakesh na maeneo ya milimani.
(AFP, DPA, Reuters)