1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watoto 600 walidhalilishwa katika Kanisa Katoliki

6 Aprili 2023

Utafiti mmoja uliofanywa kwa kipindi cha miongo sita unaonyesha kwamba zaidi ya watoto 600 katika jimbo la mashariki mwa Marekani la Maryland, walidhalilishwa na zaidi ya wahubiri 150 wa Kanisa Katoliki.

https://p.dw.com/p/4Pkz3
Kanisa/ Lisbon
Picha ya Kanisa mjini LisbonPicha: Pedro Nunes/REUTERS

Ripoti ya utafiti mmoja uliofanywa kwa kipindi cha miongo sita na iliyochapishwa jana, unaonyesha kwamba zaidi ya watoto 600 katika jimbo la mashariki mwa Marekani la Maryland, walidhalilishwa na zaidi ya wahubiri 150 wa Kanisa Katoliki.

Afisi ya mwanasheria mkuu wa Maryland iliyofanya utafiti huo kuhusu dayosisi ya Baltimore inasema imewatambua watu 156 waliohusika na udhalilishaji huo wakiwemo mapadre na walimu waliowadhalilisha watoto hao mara kadhaa. Afisi hiyo ya mwanasheria mkuu imeongeza kwamba huenda ikawa idadi hiyo ya watoto iko juu kuliko hiyo ya 600.

Akijibu yaliyomo kwenye ripoti hiyo, Askofu Mkuu wa jimbo la Baltimore William Lori ameomba radhi akisema utafiti huo unaonyesha kipindi kigumu katika dayosisi hiyo, kipindi ambacho hakitopuuzwa au kusahaulika. Katika miaka ya hivi majuzi, kumetolewa maelfu ya ripoti za udhalilishaji uliofanyiwa watoto katika miaka ya nyuma katika kanisa hilo.