1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya nyaraka 300 za siri zakutwa nyumbani kwa Trump

23 Agosti 2022

Serikali ya Marekani imekuta zaidi ya nyaraka 300 zenye alama ya siri nzito za serikali kwenye makazi ya rais wa zamani Donald Trump yaliyoko Florida.

https://p.dw.com/p/4Ftgs
CPAC-Konferenz in Texas | Donald Trump
Picha: Brandon Bell/Getty Images/AFP

Nyaraka zilizokutwa ni za shirika la ujasusi, CIA, usalama wa taifa, NSA na shirika la upelelezi wa ndani, FBI. Taarifa hii ni kulingana na gazeti la New York Times jana Jumatatu, lililonukuu vyanzo mbalimbali viliyoarifiwa kuhusu suala hilo. Lilian Mtono na taarifa zaidi.

Fungu la kwanza la zaidi ya nyaraka 150 zilizokuwa na alama ya Siri ziligunduliwa na taasisi ya kiaifa ya utunzaji wa nyaraka mwezi Januari, limeripoti gazeti hilo. Wasaidizi wa Trump waliipatia wizara ya sheria seti ya pili mwezi Juni, na seti ya tatu iligunduliwa na FBI walipovamia na kupekua makazi ya Trump mapema mwezi huu.

Hata hivyo wizara hiyo pamoja na wawakilishi wa rais huyo wa zamani hawakuwa tayari kuzungumzia mara moja ugunduzi huu wa karibuni ilipotafutwa kutoa ufafanuzi.

Soma Zaidi: Trump na washirika wake huenda walitenda uhalifu

Mapema jana, Trump aliomba mahakama ya shirikisho kuwazuia FBI kwa muda kupitia nyaraka zilizokuwa na alama ya Siri nzito ilizozikamata Agosti 8 kwenye makazi yake ya Mar-a-Lago hadi kutakapoteuliwa msimamizi maalumu wa kusimamia zoezi hilo.

USA, Palm Beach | Mar a Lago
Makazi ya Dondl Trump ya Mar-a-Lago ambako kulikamatwa nyaraka nyingine mapema mwezi AgostiPicha: mpi34/MediaPunch/picture alliance

Hoja ya Trump, iliyowasilishwa katika mahakama ya shirikisho huko West Palm Beach, Florida, pia iliitaka wizara ya sheria ya Marekani kumpatia ankara inayoonyesha kwa kina zaidi ya nyaraka zilizokamatwa na FBI kwenye nyumba yake ya Mar-a-Lago na kuwataka wachunguzi hao kurudisha vitu vyovyote ambavyo haviko kwenye kibali cha uchunguzi wao.

Msimamizi maalumu mara nyingine anaweza kuteuliwa katika kesi nyeti zaidi ili kupitia nyaraka zinazoshikiliwa na kuhakikisha wachunguzi hawapitii taarifa za upendeleo. Wakati FBI walipokuwa wakupekua nyumba za Trump, mawakili wake wa zamani Michael Cohen na Rudy Giuliani waliomba kuteuliwa kwa msimamizi huyo.

Hakimu Bruce Reinhart, kutoka West Palm Beach aliyeidhinisha kibali cha upekuzi kwenye makazi ya Trump ya Mar-a-Lago, anaangazia iwapo anaweza kuiagiza wizara ya sheria kutoa nakala iliyorekebishwa ya hati ya kiapo inayoonyesha ushahidi wa sababu za kupekuliwa kwa nyumba ya Trump.

Kukamatwa kwa nyaraka hizo ni sehemu ya uchunguzi wa FBI kuhusiana na iwapo Trump aliondoa nyaraka kinyume cha sheria wakati alipoondoka madarakani Januari 2021 baada ya kushindwa kwenye uchaguzi na rais Joe Biden kuingia mamlakani.

Trump na washirika wake walilalamika mbele ya vyombo vya habari kwamba upekuzi huo ulichochewa kisiasa.

Mashirika: RTRE