1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yulia Navalnaya kupokea Tuzo ya DW ya Uhuru wa Kujieleza

3 Mei 2024

Mjane wa hayati kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny na Wakfu wake wa Kupambana na Ufisadi, ndio washindi wa Tuzo ya 10 ya DW ya Uhuru wa Kujieleza mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/4fTSu
Reaktionen auf den Tod von Alexej Nawalny
Picha: Yves Herman/AP/picture alliance

Tuzo ya DW ya Uhuru wa Kujieleza mwaka 2024 itamuendea Yulia Navalnaya na Wakfu wa Kupambana na Ufisadi nchini Urusi, haya yametangazwa na shirika la kimataifa la utangazaji nchini Ujerumani DW siku ya Ijumaa (Mei 3).

Navalnaya ni mjane wa hayati kiongozi wa zamani wa upinzani wa Urusi - na mwasisi wa wakfu huo wa kupambana na ufisadi - Alexei Navalny.

Ataipokea binafsi Tuzo ya 10 ya Uhuru wa Kujieleza mnamo Juni 5 mjini Berlin.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner ndiye atakayetoa hotuba ya kumpongeza Navalnaya.

"Ujasiri usioyumba" wa Yulia Navalnaya

"Yulia Navalnaya amemuunga mkono mume wake Alexei navalny katika kazi yake ya kisiasa katika kupigania uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini urusi kuanzia mwanzo - licha ya hatari zote, vitisho vya kila mara na vikwazo vya kibinafsi," alisema Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg. 

"Naheshimu ujasiri wake usioyumba, dhamira yake na nguvu anayotumia kupigania Urusi iliyo huru na kusimama na wale ambao Rais wa Urusi Vladimir Putin anataka kuwanyamazisha," aliongeza Limbourg.

Mapema Aprili, Navalnaya pia alipokea Tuzo ya Uhuru ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya Ujerumani.

Navalnaya amekuwa akiongeza upinzani dhidi ya Putin, hasa tangu kifo cha mume wake katika jela nchini Urusi mwezi Februari.

Wakfu wa Kupambana na Ufisadi ni nini?

Navalny aliuanzisha wakfu huo mwaka 2011 lengo likiwa kupamba na ufisadi nchini Urusi kwa kuchunguza visa vya ufisadi na kufanya utafiti kuhusiana na wakuu wa kisiasa nchini Urusi.

Ujerumani I Yulia Navalnaya akiwa mjini Berlin - 2024
Yulia Navalnaya akiwa mjini Berlin 2024Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture

Mamlaka nchini Urusi zililipiga marufuku shirika hilo mwaka 2021, ila likaibuka kimataifa mwaka mmoja baada kuendeleza mapambano hayo. Urusi inalitaja shirika hilo kama "shirika la itikadi kali."

Wakfu huo wa Ufisadi huchapisha matokeo ya uchunguzi wake katika chaneli ya YouTube ya Navalny. Shirika hilo lilianzisha orodha ya wale iliowaitwa "watoaji rushwa na wachochezi wa vita" ambao ni wandani wa Putin waliothibitishwa kushawishi siasa, biashara na benki za Urusi kifisadi kwa niaba ya rais huyo wa Urusi.

Bodi ya ushauri ya wakfu huo inawajumuisha Mbunge wa bunge la Ulaya na Waziri Mkuu wa zamani wa Ubelgiji Guy Verhofstadt, mwandishi ambaye ni mshindi wa Tuzo wa Pulitzer Anne Applebaum na mwanasayansi wa kisiasa Francis Fukuyama.

Kamatakamata ya waandishi nchini Urusi

Tuzo hii inatolewa wakati ambapo wanahabari wa Urusi wanakamatwa kwa kiasi kikubwa.

Siku chache kabla tangazo la DW, polisi ya Urusi ilimkamata mwandishi wa habari Konstantin Gabov, ambaye aawali alikuwa anafanya kazi kama ripota wa DW, pamoja na mpiga picha wake Sergei Karelin.

Mamlaka za Urusi zilisema kamatakamata hiyo ilikuwa sehemu ya kukabiliana na masuala itikadi kali, kwani iliwatuhumu kwa kukusanya taarifa kwa ajili ya chaneli ya YouTube ya Wakfu wa Kupambana na Ufisadi wa Navalny.

Lakini mashtaka waliyofunguliwa hayahusiani na kazi waliyokuwa wakifanya kama waandishi wa DW, shirika la utangazaji la Ujerumani ambalo limepigwa marufuku nchini Urusi.

Tuzo ya DW ya Uhuru wa Kujieleza ni nini?

Tangu mwaka 2015, Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya DW imekuwa ikitolewa kwa mwandishi au mpango ulioonesha juhudi kubwa za kusimamia uhuru wa haki hasa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Mwanablogu wa Saudi Arabia Raif Badawi alikuwa mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya DW.

Mwaka uliopita, mwandishi aliyezaliwa El-Salvador Oscar Martinez, ambaye ni mhariri mkuu wa gazeti la mtandaoni la El Faro, alituzwa kutokana na kazi yake.

GMF 2023 | Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza | Mshindi Oscar Martinez
Oscar Martinez akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter LimbourgPicha: Bjorn Kietzmann/DW

Mwandishi wa shirika la habari la Associated Press AP na mwandishi wa kitabu Mstyslav Chernov pamoja na mpiga picha wa kujitegemea Evgeniy Maloletka, walituzwa kutokana na kazi yao ya kuviangazia vita vya Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.

Hafla ya Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza kwa kawaida ndicho kilele cha Kongamano la Dunia la Waandishi wa Habari linaloandaliwa na DW kila mwaka mjini Bonn, Ujerumani.

Chanzo: https://www.dw.com/en/yulia-navalnaya-to-receive-dw-freedom-of-speech-award-2024/a-68951639