1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani

Admin.WagnerD30 Oktoba 2018

Idadi ya viumbe hai na ikolojia ulimwenguni imeporomoka kwa viwango vibaya kabisa katika kipindi cha miongo minne iliyopita imesema ripoti ya fuko la uhifadhi wanyamapori WWF iliyotolewa leo.

https://p.dw.com/p/37OIi
Arktischer Ziesel
Picha: picture alliance/WILDLIFE/H. Schweiger

Ripoti hiyo imeonesha kuwa idadi kubwa ya viumbe imepotea kutokana na uchu wa binadamu na shughuli zake na hali hiyo inayotishia ustawi wa siku za usoni. 

Data za ripoti hiyo mpya ilopewa jina sayari hai au´the living planet´ zinaonesha kuwa kwa jumla idadi ya wanyama walio na uti wa mgongo inayojumuisha ndege, amfibia, reptilia, samaki na mamalia imepungua kwa asilimia 60 tangu mwaka 1970.

WWF imesema idadi ya viumbe vinavyoishi kwenye maji baridi hususan samaki imeporomoka kwa wastani wa asilimia 83 kutokana na shughuli za ujenzi wa mabwawa makubwa, uvuvi uliopindukia, ongezeko la watu duniani pamoja na magonjwa yanayowakabili.

Amerika ya kati na kusini athari ni kubwa zaidi.

Brasilien Jamanxim Nationalpark Brandrodung Regenwald
Picha: Getty Images/AFP/A. Scorza

Ikolojia ya eneo la ukanda wa kitropiki la amerika ya kati na kusini inakopatikana pia misitu ya amazon ndiyo imeathirika zaidi kwa wastani wa asilimia 89 sababu kubwa ikiwa ni ukataji miti uliokithiri

Kulingana na WWF tangu mwaka 1500 shughuli za kilimo na uvunaji uliofurutu ada wa wanyama umekuwa sababu ya kupotea kutoka uso wa dunia kwa hadi asilimi 75 ya viumbe jamii ya mamalia, ndege, reptilia, amfibia na mimea.

Kitisho kingine kilichoangaziwa na ripoti hiyo ni suala la makaazi ya viumbe ambapo takwimu mpya zinaonesha ni robo pekee ya eneo la ardhi duniani lililobaki katika hali ya asili huku maeneo ya ardhi oevu yakipungua kwa hadi asilimia 87 kutokana na watu kujenga juu ya maeneo hayo, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi.

Matumbawe na wadudu wachavushaji hatarini kutoweka

Mexiko Korallenriff
Picha: DW/S. Meinecke

Ongezeko la joto linalotokana na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa pia limegeuka kitisho kikubwa kwenye ikolojia ya bahari ambapo kiasi nusu ya matumbawe ambayo ndiyo chanzo cha uhai kwa hadi robo ya viumbe vya baharini imepotea.

Jopo la Umoja wa mataifa lilionya mwezi uliopita kuwa hata ikiwa ulimwengu utafanikiwa kupunguza ongezeko la joto kwa kiwango cha nyuzi 1.5 kipimo cha selshesi bado itakuwa kuwa jambo gumu kuzuia kupotea kwa matumbawe.

WWF imeorodhesha pia wasiwasi wa kupotea kwa viumbe vinavyosaidia uchavushaji mimea ikiwemo nyuki, nondo, vipepeo, popo na jamii nyingine za ndege kutokana na matumizi makubwa ya dawa  za kuua wadudu na kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi kuwa miji.

Ripoti hiyo imetoa wito wa hatua za dharura kukabiliana na hali hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo ikiwa ulimwengu utahitaji kuokea viumbe hai na baianui.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/DW Eng.

Mhariri: Saumu Mwasimba