Mataifa ya kiislamu yahimizwa kushirikiana zaidi kibishara
19 Desemba 2019"Ulimwengu wa kiislamu unapaswa kuwa na mikakati ya kujiokoa kutoka kwa utegemezi wa fedha za Marekani” alisema Rouhani katika ufunguzi wa mkutano wa Kiislamu unaofanyika Mjini Kuala lumpur Malaysia kama jukwaa, kulaani vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi yake. huo wa siku tatu uliowajumuisha pia viongozi kutoka Qatar na mwenyeji Malaysia.
Katika mkutano huo Rouhani amependekeza kuundwa kwa benki maalum na uwepo wa utaratibu wa kifedha miongoni mwa mataifa ya kiislamu, kutumia sarafu za nchi zao na kupeana nafasi za ushirikiano zaidi wa kibiashara.
Amesema kuongezeka kwa makundi ya itikadi kali pamoja na changamoto kadhaa kama serikali dhaifu, umasikini na rushwa ni mambo yanayohatarisha uhuru wa mataifa yao na kutoa nafasi kwa mataifa ya Magharibi kuingilia mizozo kama ilivyo fanya nchini Syria, Yemen, Afghanistan na mataifa mengine ya kiislamu huku akitolea mwito mataifa hayo kuungana pamoja kukabilian na matatizo yaliopo.
Rais Erdogan aikosoa Jumuiya ya Kiislamu OIC
Kwa upande wake rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliikosoa Jumuiya ya nchi za kiislamu OIC akiuambia mkutano huo kwamba jukwaa hilo linalopaswa kuwaleta waislamu pamoja limeshindwa kutatua masuala yanayowakabili.
Erdogan amesema mpaka sasa tatizo la Palestina limeshindwa kutatuliwa, Jumuiya hiyo pia imeshindwa kuzuwiya unyonyaji wa rasilimali za mataifa ya kiislamu na kutozuwia kugawika kwa mataifa hayo kufuatia migogoro ya kimadhehebu.
Huku hayo yakiarifiwa waziri mkuu wa Malaysia Mahathir Mohamad amewaeleza viongozi waliokuwa katika mkutano huo kwamba wanapaswa kukabiliana na chuki dhidi ya waislamu pamoja na kushughulikia changamoto zinazowakabili waislamu wote ulimwenguni.
Saudi Arabia hata hivyo haikuhudhuria mkutano huo kwa hoja kwamba haukuandaliwa chini ya misingi ya Jumuiya ya nchi za kiislamu. Pakistan pia imeususia mkutano huo kama njia ya kuiunga mkono Saudi Arabia ambayo ni mshirika wake.
Vyanzo: afp, Reuters