1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito kusaidia wakimbizi wa Irak

p.Martin25 Septemba 2007

Nchini Iraq kuna hatari ya kuzuka maafa makubwa ya kiutu,lakini hali hiyo haipewi kipaumbele na jumuiya ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/CH7j

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika linalotetea haki za binadamu duniani-Amnesty International.

Ripoti hiyo inasema,jumuiya ya kimataifa na hasa zile nchi zilizosababisha kuanza kwa machafuko nchini Irak,zinapaswa kuchukua hatua za dharura kuwapatia wakimbizi makazi mapya na kuzisaidia nchi zilizopokea wakimbizi kutoka Irak.

Mkurugenzi-mtendaji wa Amnesty International, bwana Larry Cox anasema,jumuiya ya kimataifa na hasa Marekani,ina wajibu wa kiadilifu kuwalinda na kuwasaidia zaidi wakimbizi wa Kiiraki. Ispofanya hivyo,kutazuka maafa makubwa zaidi ya kiutu na machafuko ya kisiasa huenda yakaongezeka katika kanda hiyo.

Ingawa hakuna takwimu rasmi,inatathminiwa kuwa kiasi ya Wairaki milioni 4.2 wanaishi ukimbizoni. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi duniani,UNHCR,kila siku moja,kama Wairaki 2,000 hupoteza maskani zao.Nchi za jirani Syria na Jordan ndio zinabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kutoka Irak.

Kwa mfano,nchini Jordan kuna kati ya wakimbizi 500,000 hadi 750,000 hali iliyoifanya nchi hiyo kuchukua hatua ya kuimarisha sheria za uhamiaji. Hata Syria iliyo na wakimbizi milioni 1.4-ikiwa ni sawa na asilimia 8 ya umma wa nchi nzima,hivi karibuni pia ilipitisha sheria mpya za uhamiaji. Lakini kwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani,sheria hizo zimewekwa kando.

Azma ya sheria hizo ni kuipunguzia serikali ya Damascus,gharama za kuwapatia wakimbizi wa Kiiraki,maskani,chakula pamoja na huduma za elimu na afya.Syria na Jordan zimesifiwa na Amnesty International kwa misaada iliyotolewa kwa wakimbizi wa Kiiraki hadi hivi sasa,lakini jumuiya ya kimataifa na hasa Marekani imelaumiwa vikali.

Ingawa serikali ya Marekani imeashiria kuwa itaongeza idadi ya wakimbizi wa Kiiraki watakaopokewa nchini Marekani,ripoti ya Amnsety International inasema,idadi iliyopendekezwa ni ndogo mno kulinganishwa na ule uwezo wa Marekani.

Kwa hivyo katika juhudi ya kurekebisha kasoro za sera za hivi sasa za Marekani kuhusu wakimbizi wa Kiiraki,wabunge wa nchi hiyo wamependekeza mswada unaotoa mwito wa kuharakisha utaratibu wa kuwapatia Wairaki hadhi ya ukimbizi,kwa kufungua ofisi itakayoshughulikia maombi ya ukimbizi,mjini Baghdad.Vile vile Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani itaombwa kujitahidi kutoa msaada kwa nchi zinazopokea wakimbizi kutoka Irak.

Hata Umoja wa Mataifa umekosolewa kuwa unajiburura kushughulikia wakimbizi wanaotokea Irak.Umoja huo umelaumiwa kuwa hautoi msaada wa kutosha wa fedha na isipokuwa kwa shirika la UNHCR,mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa hayajishughulkishi sana na tatizo la wakimbizi wa Kiiraki.