1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

William Tubman: Mwanamageuzi wa Liberia

Yusra Buwayhid
11 Februari 2020

Liberia, taifa la watumwa walioapata uhuru, liljengwa kwa kuwakandamiza watu wake wa asili. William Tubman alipochaguliwa rais aliwaunganisha watu wake. Aliitaka iwe na mustakbali mzuri, ila hakufanikiwa.

https://p.dw.com/p/3Xazt
DW African Roots | William Tubman

William Tubman: Mwanamageuzi wa Liberia

Ni lipi chimbuko la William Tubman?

William Vacanarat Shadrach Tubman alizaliwa Novemba 29, 1895. Ametokea Kusini mashariki mwa Liberia, katika mji unaoitwa Harper ulioko Kaunti ya Maryland. Haikuwa kwa bahati mbaya kwamba majina mengi ya watu na maeneo ya nchini Liberia yanalingana na yale ya nchini Marekani: Jamhuri ya Liberia ilianzishwa mwaka 1847 na watumwa walioachiliwa huru kutoka Marekani. Waliwasili nchini humo katika makundi tofauti mwanzoni mwa karne hiyo. Wazazi wa baba yake Tubman walikuwa ni miongoni mwa kundi la watumwa 69 walioletwa Liberia 1844. Mama yake alizaliwa Atlanta, Georgia nchini Marekani.

Tubman alilelewa na Baba mkali katika kuwafundisha watoto wake nidhamu. Aliyekuwa akifanya kazi tofauti; mvunja wame, jenerali wa jeshi na pia mhubiri wa madhehebu ya Kikiristo ya Umethodisti. Alimtaka Tubman na ndugu zake wote kuhudhuria ibada ya kila siku ya maombi ya familia na aliwalazimisha kulala chini kwenye sakafu kwa sababu akiamini vitanda ni "vilaini sana na vinamharibu mtu tabia".

Kipi kilichompa William Tubman umaarufu?

William Tubman: Mwanamageuzi wa Liberia

Tubman ambaye alikuwa rais wa Liberia karne ya 19 kuanzia 1944 hadi kifo chake 1971, mara nyingi anaelezwa kama baba wa Liberia ya kisasa. Kupitia uwekezaji wa kigeni, alijenga barabara nyingi za Liberia, njia za reli pamoja na kuikarabati bandari ya Monrovia, na kutengeneza miundombinu ya kusafirishia nje ya nchi mpira na madini ya chuma. Wakati wa kifo chake, Liberia ilikuwa na idadi kubwa duniani ya meli za kusafirishia biashara. Majengo mengi ya kiserikali kama vile Jengo la Capitol, Jumba la Jiji la Monrovia au Kituo cha Utamaduni cha kitaifa kinachojulikana sasa kama Kendeja yalijengwa wakati wa Tubman. Pia alijenga hoteli ya kwanza ya kimataifa kwa jina la Ducor mjini Monrovia. Ilikuwa pia ni hoteli ya kwanza ya kifahari yenye nyota tano Afrika Magharibi.

DW African Roots | William Tubman
Asili ya Afrika | William Tubman

Je, Tubman alifanikiwa kuhakikisha watu wake wanaishi maisha mazuri?

Wakati wa uongozi wa Tubman, Liberia ilinawirika. Serikali yake pia iliwekeza katika sekta ya elimu na afya. Liberia pia ilianzisha mpango wa kusoma na kuandika unaotumia mbinu inayojulikana kama "Kila mmoja amfundishe mmoja". Labda muhimu zaidi, William Tubman alijitahidi kuwaunganisha watu wa Liberia. Baada ya karne moja, watu wa asili wa Liberia walinyanyaswa na Waliberia waliotokea Marekani waliokuwa wa tabaka la juu, serikali ya Tubman alilazimisha haki sawa kwa wote.

Hata hivyo, uongozi wa Tubman wa miaka 27 ulikuwa ukikosolewa. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka miaka ya 1980 vilisababaisha misingi ya nchi hiyo iliyoanzishwa na Tubman kutiliwa shaka. Mara nyingi alikuwa akikosolewa kwa kuendesha nchi kiimla na kuishi maisha ya kifahari. Baadhi ya watu pia wakihofia uhusiano wake wa karibu na Marekani huenda ukahatarisha uhuru wa Liberia.

DW African Roots | William Tubman
Asili ya Afrika | William Tubman

Kuheshimu mchango wake wa kuleta mafanikio Liberia, siku ya kuzaliwa ya Tubman inaadhimishwa nchini humo kama likizo ya kitaifa.

Je! Ni nukuu gani maarufu za William Tubman zinazokumbukwa ?

"Liberia haikufaidika na matunda ya ukoloni"

"Hatutangazi vita dhidi ya ujamaa ikiwa utabakia miongoni watu ambao wanaouunga mkono, lakini tutapigana hadi kufa dhidi ya jaribio lolote la kutaka kutulazimisha sisi kile tunachodhani ni udanganyifu wa ajabu".

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.