1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Widodo achaguliwa tena rais wa Indonesia

21 Mei 2019

Rais wa Indonesia Joko Widodo amechaguliwa kuongoza kwa awamu ya pili baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi  kuonyesha amepata asilimia 55.5. Hata hivyo, mpinzani wake Prabowo Subianto ameapa kupinga mahakamani ya juu.

https://p.dw.com/p/3IofF
Wahlen in Indonesien   Joko Widodo
Picha: Reuters/E. Su

Kulingana na tume ya uchaguzi Widodo ameshinda kwenye majimbo 21 kati ya 34, kwa jumla ya kura milioni 85.6, dhidi ya Subianto aliyepata kura milioni 68.5.

Zoezi la kuhesabu kura lilimalizika rasmi usiku wa jana na tume ya uchaguzi nchini humo ikatangaza matokeo mapema hii leo. Matokeo hayo yalimuonyesha rais Widodo kuongoza kwa asilimia 55.5 ya kura zote, akifuatiwa na Generali huyo wa zamani Subianto na anayejifungamanisha na Waislamu wenye itikadi kali aliyepata asilimia 45.5.

Indonesien Yogyakarta - Präsidentschaftswahl
Vituo vya kupigia kura vikiwa vimenakshiwa kwa rangi za kuvutiaPicha: picture-alliance/NurPhoto/R. Hamiid

Maelfu ya polisi na wanajeshi walikuwa katika tahadhari kubwa katika mji mkuu Jakarta, wakitarajia kuzuka kwa maandamano ya wafuasi wa Subianto. Ofisi za makao makuu ya tume ya uchaguzi zilizoko katikati ya mji wa Jakarta zimezungushiwa nyaya za umeme na ulinzi mkali.

Alipozungumzia ushindi huo, Widodo amesema yeye pamoja na mgombea mwenza wake, kiongozi wa dini mhafidhina, Ma'ruf Amin watakuwa rais na makamu wa rais wa watu wote wa Indonesia.

Indonesien wählt neuen Präsidenten und Parlament | Joko Widodo und Prabowo Subianto
Prabowo Subianto(pichani kulia) ameahidi kupinga matokeo hayo mahakamaniPicha: picture-alliance/AP Photo

Subianto ambaye pia alishindwa kwenye uchaguzi wa 2014 dhidi ya Widodo na kujaribu bila mafanikio kupinga matokeo mahakamani amedai kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye uchaguzi lakini hajatoa kithibitisho chochote cha msingi.

Wakaazi wa Jakarta nao wameyapokea matokeo hayo kwa hisia tofauti, hasa kufuatia madai hayo ya Subianto. Ahmad Djunaedi alisema "Nadhani wanatakiwa kwenda mahakama ya katiba, kama wana mashaka na matokeo hayo, kwa sababu mahakama ya katiba ipo kwa ajili ya kusuhisha madai yoyote ya uchaguzi. Waende mahakamani kwanza, kisha sisi raia tutasubiri maamuzi ya mahakama".

Afisa wa kampeni za Subianto Sufmi Dasco Ahmad amesema watawasilisha kesi hiyo kwenye mahakama ya katiba katika kipindi cha siku tatu. Widodo ameeleza kuridhishwa na namna mpinzani wake huyo anavyochukua hatua za kupinga matokeo hayo kwa kuzingatia katiba na sheria.

Awali Subianto na wafuasi wake walitishia kuingia mitaani kupinga matokeo hayo kwa kutumia nguvu ya umma badala ya kwenda mahakamani kwa sababu hawana imani kama mahakama hiyo itatenda haki.

Waangalizi huru na wachambuzi wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki, ingawa Prabowo na timu yake ya kampeni wanaibua madai hayo ya udanganyifu.

Iwapo mahakama itapata vithibitisho vya kutosha kufungua kesi hiyo, inatakiwa kutoa uamuzi katika kipindi cha siku 14 baada ya nyaraka zote kuwasilishwa na wadai. Uamuzi wa mahakama hiyo ni wa mwisho na haukatiwi rufaa.