1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kanda ya Afrika kujadili kitisho cha ugonjwa wa Mpox

26 Agosti 2024

Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani, WHO inaanza mkutano wake wa siku tano katika Jamhuri ya Kongo kujadili kitisho cha ugonjwa wa Mpox.

https://p.dw.com/p/4jvMe
Mgonjwa wa mpox.
Mgonjwa wa Mpox.Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus na mkurugrnzi wa Kanda ya Afrika ya WHO, Matshidiso Moeti, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo unaoanza leo Jumatatu, pamoja na mawaziri 47 wa afya kutoka katika eneo hilo.

Kulingana na tovuti ya Shirika la Afya Duniani, ajenda ya mkutano huo wa kilele wa Congo-Brazzaville, ni pamoja na maandalizi ya dharura ya afya, jinsi nchi za Afrika zitakavyosaidiwa kukabiliana na Mpox, na maendeleo ya huduma ya afya kwa wote.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Tedros amesema ushirikiano wa kimataifa unahitajika.

"Ni wazi kwamba mwitikio ulioratibiwa wa kimataifa ni muhimu kuumaliza mripuko huu na kuokoa maisha. Dharura ya afya ya umma na wasiwasi wa kimataifa ni kiwango cha juu zaidi cha tahadhari kulingana na sheria ya kimataifa ya afya." amesema Ghebreyesus.

Mkutano huo unafanyika siku chache baada ya WHO na Vituo vya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Afrika, CDC, kuomba msaada wa kifedha, ushirikiano zaidi wa kina, na ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na mripuko wa homa ya Mpox.

WHO imetoa kiasi cha dola milioni 1.5 kutoka kwenye mfuko wa dharura ili kuushughulikia ugonjwa wa Mpox, na inatarajiwa kutoa fedha zaidi, pamoja na kupata fedha kutoka kwa nchi wafadhili. Hata hivyo, Tedros amesema mpango wa kimkakati wa kujiandaa na kukabiliana na Mpox, unahitaji dola milioni 135 za awali.

Nchi za Afrika zimeongezea ufuatiliaji na hatua za kudhibiti, wakati mripuko huo ukienea zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na nchi hiyo ikijiandaa kuanza kutoa chanjo ndani ya wiki hii, ikiwa zitafika kwa wakati.

Mpox yaendelea kusambaa mataifa zaidi ya Afrika huku chanjo zikisubiriwa 

Chanjo ya Mpox
Chanjo ya Mpox. Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, Uganda imethibitisha visa viwili zaidi vya Mpox, na kuifanya idadi jumla ya wagonjwa wa homa hiyo kufikia wanne katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Uganda, Henry Mwebesa, amesema leo kuwa wagonjwa wawili wameambukizwa kirusi cha Clade 1b, ambacho kimezusha wasiwasi wa kimataifa.

Ama kwa upande mwingine, visa 21 vya homa ya Mpox vimerekodiwa Congo-Brazzavile. Waziri wa Afya wa Congo-Brazzavile, Gilbert Mokoki, jana aliiambia televisheni ya taifa kuwa nchi hiyo imerekodi visa 158 vinavyoshukiwa kuwa vya Mpox tangu kuanza kwa mwaka huu, huku 21 vikiwa vimethibitishwa. Kulingana na Mokoki, visa vya hivi karibuni ni viwili ambavyo viliripotiwa siku ya Alhamisi.

Gabon nayo imerekodi kisa cha kwanza cha Mpox, ingawa wizara ya afya haijaeleza wazi aina ya kirusi kilichogunduliwa kwa mgonjwa huyo.

Huku hayo yakijiri, dozi za kwanza 10,000 za chanjo ya Mpox zinatarajiwa kuwasili Afrika wiki ijayo.

Aidha, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewaombea walioathirika na virusi vya Mpox, akisema kuwa homa hiyo imekuwa dharura ya kimataifa ya afya.

Akizungumza mwishoni mwa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Mt. Peter, Papa Francis amesema anawaombea wote walioambukizwa homa hiyo, hasa watu wa Kongo, ambao wameathiriwa zaidi.