1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Hospitali 20 kati ya 36 za Gaza hazifanyi kazi tena

10 Novemba 2023

Shirika la Afya Duniani WHO, limesema leo kuwa hospitali 20 kati ya 36 katika Ukanda wa Gaza hazifanyi kazi kwa sababu ya mashambulizi makali, uharibifu na ukosefu wa vifaa vya matibabu.

https://p.dw.com/p/4YgQ8
Hospital in Gaza
Picha: DW

Msemaji wa WHO Margaret Harris amesema hata zile hospitali zinazofanya kazi zinatoa tu huduma za dharura, kwa kuwa nyingi zimekosa dawa za kutosha za kuua vijidudu, dawa za ganzi na umeme kuwezesha utoaji huduma kwa njia ya kawaida kwa wagonjwa.

Israel na Hamas wapambana karibu na hospitali mbili kwenye mji wa Gaza

"Na sijapata taarifa ya hospitali ya Al-Shifa kwa sasa, lakini tunajua wanakabiliwa na mashambulizi makubwa na hospitali ya Rantisi ambayo ndiyo pekee inayotoa huduma kwa watoto kaskazini mwa Gaza. Na katika hospitali hiyo kulikuwa na watoto kadhaa ambao walikuwa kwenye machine za kupumua na watoto kwenye machine za kusafisha figo, hali ambayo huwezi kuwahamisha hadi maeneo salama," alisema Margaret Harris.

Wakati hayo yakijiri, wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na kundi la wanamgambo la Hamas limesema idadi ya vifo katika ukanda huo imepindukia 11,078.