1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Ebola inaweza kusambaa kirahisi DRC

16 Agosti 2018

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, yanakwamisha juhudi za kupambana na mripuko wa ugonjwa wa Ebola nchini humo.

https://p.dw.com/p/33Fjv
Genf Tedros Adhanom Ghebreyesus, Generealdirektor WHO | Ebola-Ausbruch Kongo
Picha: Reuters/D. Balibouse

Kutokana na mgogoro huo, shirika hilo limetoa wito wa kusitishwa mapigano ili kuzuia virusi vya Ebola kusambaa kwa urahisi. Wakati idadi ya watu waliokufa tangu kuzuka kwa Ebola Agosti Mosi katika jimbo la Kivu Kaskazini ambalo linakabiliwa na vurugu ikiwa imefikia 41, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ana wasiwasi kwamba hali iliyoko kwenye jimbo hilo, imesababisha mazingira rahisi ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Tedros ambaye hivi karibuni aliyazuru maeneo ya Beni na Mangina yaliyokumbwa na Ebola, amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba alikuwa na hofu kabla ya ziara yake hiyo, lakini kwa sasa ana wasiwasi zaidi.

Kongo Armee sucht nach Milizenchef Bosco Ntaganda
Wanajeshi wa Kongo wanaopambana na makundi yenye silaha KongoPicha: dapd

''Kinachoufanya mripuko wa Ebola Mashariki mwa Kongo au Kivu Kaskazini kuwa hatari zaidi ni kutokana na changamoto ya usalama, kuna mzozo unaoendelea. Usiku tuliolala Beni, kulikuwa na mapigano ndani ya umbali wa kilomita 15 na raia wanne waliuawa na watu wengine walitekwa nyara. Kwa hiyo mazingira ni mazuri kwa Ebola kusambaa kwa urahisi,'' alisema Tedros.

Mripuko wa Ebola katika mkoa wa Beni, ambao unapakana na Uganda na Rwanda, ulitangazwa wiki moja baada ya Shirika la Afya Duniani na serikali ya Kongo kupongeza hatua ya kumalizika kwa ugonjwa huo uliozuka kwenye jimbo la kaskazini magharibi la Equateur, na kusababisha vifo vya watu 33.

Mripuko wa sasa wa Ebola ambao umeshuhudia visa 57 vya maambukizi ambapo watu 30 wamethibitishwa na 27 wanadhaniwa kuwa huenda wameambukizwa, ni wa kumi kutokea tangu mwaka 1976, wakati ugonjwa huo ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Kongo karibu na Mto Ebola.

Maafisa wa afya wamesema kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa ugonjwa huo, kifo kimoja kimethibitishwa katika jimbo jirani la Ituri. Lakini katika jimbo la Kivu Kaskazini maafisa wa afya wanalazimika kusafiri ili kutekeleza majukumu yao miongoni mwa zaidi ya makundi 100 yenye silaha na Tedros anasema kwamba kuna visa 120 vya ghasia ambavyo vimeripotiwa tangu mwezi Januari. Aidha, mkurugenzi huyo wa WHO, ameyatolea wito makundi yanayohasimiana kusitisha mapigano, kwa sababu virusi vya Ebola ni hatari kwa wote.

Kongo Ebola
Maafisa wa afya wa Kongo katika juhudi za kupambana na EbolaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Katika juhudi za kupambana na Ebola, maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameanza kutumia dawa ya majaribio ya kutibu ugonjwa wa Ebola inayojulikana kama mAb114. Wizara ya afya ya Kongo, imesema kuwa hii ni mara ya kwanza dawa hiyo kutumika tangu ugonjwa huo ulipozuka.

Wakati huo huo, watu 127 wamekufa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu tangu mwezi Februari, huku vifo vingine 22 vikiwa vimetokea Niger. Waziri wa Afya katika Jimbo la Kasai Mashariki, Hippolyte Mutombo Mbwebwe, amesema jumla ya wagonjwa 2,100 kwa sasa wanatibiwa na tangu mwezi Februari vifo 125 vimeripotiwa. Visa vingine 10, vikiwemo vifo viwili, vimethibitishwa katika jimbo jirani la Kasai ya Kati.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman