1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WFP yasitisha usambazaji wa chakula kaskazini mwa Gaza

20 Februari 2024

Israel imeendeleza mashambulizi yake huko Gaza ambapo kundi la Hamas limesema zaidi ya watu 100 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

https://p.dw.com/p/4cdE9
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP
Nembo ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFPPicha: Million Hailesilassie/DW

Akihudhuria mkutano wa waarabu wa maendeleo endelevu mjini Cairo, Mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiarabu Ahmed Aboul Gheit, ameonya kuhusu athari za kile alichokiita "uharibifu uliokusidwa" huko Gaza: 

"Tunakutana leo katika ukumbi huu wa kihistoria katikati ya hali mbaya inayosababisha huzuni na hasira kutokana na kile ambacho ndugu zetu wa Palestina wanakabiliana nacho kutoka kwa mvamizi ambaye anatumia uwezo wake wote kutokomeza azma ya Palestina. Inabidi niseme kwamba, athari za uharibifu huu uliokusudiwa na unaofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, ambao unateketeza mambo yote muhimu kwa ajili ya maisha ya binaadamu, zitaendelea kushuhudiwa kwa miongo kadhaa ijayo," alisema Gheit.

Vita vya Israel-Hamas vyazua mvutano tamasha la Berlinale

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza  kusitisha usambazaji wa bidhaa muhimu za chakula kaskazini mwa ukanda wa Gaza hadi pale hali ya usalama itakaporuhusu tena kuendelea kwa zoezi hilo. 

Kulingana na ripoti ya shirika huru la watafiti kutoka Marekani na Uingereza, watu zaidi ya 8,000 wako hatarini kufariki katika miezi sita ijayo huko Gaza, kutokana na mparaganyiko katika mfumo wa afya.