1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WFP yaonya mzozo wa Ukraine na Urusi huenda ukaithiri Yemen

25 Februari 2022

Shirika la WFP, limeonya kuwa mzozo kati ya Urusi na Ukraine huenda ukaongeza bei ya mafuta na chakula nchini Yemen na kusababisha watu wengi zaidi kukumbwa na njaa huku ufadhili wa misaada ukipungua.

https://p.dw.com/p/47aMh
Symbolbild I World Food Program (WFP) in Afghanistan
Picha: Mohammad Jan Aria/ Xinhua/picture alliance

Tangazo la shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani, WFP,  limekuja wakati Urusi ikifanya uvamizi kamili dhidi ya Ukraine na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta kupita dola 100 kwa pipa. Bei ya ngano barani Ulaya pia ilipanda kwa kiasi kikubwa kwa matarajio ya usambazaji wa chini wa bidhaa hiyo, kwani Ukraine na Urusi ni wazalishaji wakubwa zaidi wa bidhaa hiyo duniani.

Katika taarifa siku ya Alhamisi, WFP imesema kuwa mzozo huo nchini Ukraine huenda ukaongeza zaidi bei ya mafuta na chakula hasa nafaka katika taifa hilo linalotegemea uagizaji bidhaa kutoka nje. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa bei ya chakula imeongezeka zaidi ya mara mbili  katika maeneo mengi nchini Yemen katika muda wa mwaka mmoja uliopita na kuacha zaidi ya nusu watu wa taifa hilo wakihitaja msaada wa chakula na kuongeza kuwa bei ya juu ya chakula itasukuma watu zaidi katika hali mbaya zaidi ya njaa na utegemezi wa misaada ya kibinaadamu.

WFP yaonya kushindwa kuwalisha wanaokabiliwa na baa la njaa katika wiki zijazo

WFP imeonya mara kwa mara kwamba fedha za ufadhili zimekuwa zikipungua licha ya Yemen kupitia kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita mzozo mbaya zaidi wa kibinaadamu duniani. Taarifa hiyo imemnukuu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la WFP, David Beasley, akisema kuwa hawana la kufanya ila kuchukuwa chakula kutoka kwa wenye njaa ili kuwalisha wanaokabiliwa na baa la njaa na kuongeza kuwa iwapo hawatapata ufadhili wa haraka katika wiki chache zijazo, wanakabiliwa na hatari ya kukosa kuwalisha hata hao wanaokabiliwa na baa la njaa.

Yemen Huthi Kämpfer
Wafuasi wa kundi la Kithouthi nchini YemenPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Huku hayo yakijiri, taarifa kutoka kwa wizara ya fedha ya Marekani imesema siku ya Jumatano kwamba imewawekea mtandao wa kimataifa unaofadhili vita vya kundi la Kihouthi dhidi ya serikali nchini Yemen na kuongeza mashambulizi makali yanayozidi kutishia raia na miundombinu ya kiraia katika mataifa jirani.

Wizara hiyo imeendelea kusema kwamba mtandao huo unaoongozwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu - Quds, lililoorodheshwa na Marekani kama wafadhili wa kundi la Kihouthi pamoja na mfadhili mmoja wa kundi hilo, Said al-Jamal, umehamisha mamilioni ya dola nchini Yemen kupitia mtandao tata wa kimataifa wa makundi yanayounga mkono mashambulizi ya Kihouthi.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba vita nchini Yemen vimesababisha vifo vya watu 377,000 kufikia mwisho wa mwaka 2021, kupitia njia za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za njaa na magonjwa.