1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wenyeji Cameroon wasonga hatua ya mtoano michuano ya AFCON

18 Januari 2022

Wenyeji wa michuano ya kandanda ya mataifa ya Afrika, AFCON, timu ya Cameroon imefanikiwa kusonga mbele kwenda hatua ya 16 bora kufuatia mchezo wake na timu ya taifa ya Cape Verde uliomalizika kwa tasa ya bao 1-1.

https://p.dw.com/p/45fLx
Kamerun Yaoundé | Afrika-Cup | Kamerun v Kap Verde
Picha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Alikuwa ni kapteni wa timu ya Cameroon Vincent Aboubakar aliyezitikisa nyavu za Cape Verde mnamo dakika ya 39 baada ya timu zote mbili kuonesha kandanda safi tangu mwanzo wa mchezo.

Hilo lilikuwa goli la tano katika michuano hii ya AFCON la kiungo huyo anayecheza soka la kulipwa nchini Saudi Arabia na ambaye atatimiza miaka 30 Jumamosi inayokuja.

Aboubakar ni mchezaji wa kwanza wa Cameroon kupachika mabao kwenye michezo yote mitatu ya hatua ya makundi katika kombe la mataifa ya Afrika. Rikodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Samuel Eto'o aliyefunga magoli 5 kwenye michuano ya AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana.

Baada ya bao hilo, wachezaji wa Cape Verde walionesha kuhamaki na kuanzisha mashambulzii makali kuelekea lango la Cameroon wakinuwia kusawazisha lakini hawakuambulia kitu hadi dakika 45 za kwanza za mchezo zilipomalizika.

Cape Verde wasawazisha kipindi cha pili 

Kamerun Yaoundé | Afrika-Cup | Kamerun v Kap Verde
mchezo kati ya Cameroon na Cape Verde Picha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Katika kipindi cha pili taifa hilo la kisiwa lilimuingiza mshambuliaji wake Garry Rodrigues na alifanikiwa kuisawazishia timu yake ndani ya dakika nane za kwanza.

Cameroon ilikuwa nusura wapate bao jingine katika kipindi cha pili kupitia kapteni wake Aboubakar lakini hilo halikufanikiwa baada ya mpira kuwaponyoka ndani ya kumi na nane za lango la Cape Verde.

Matokeo hayo ya 1-1 yanaipatia nafasi timu ya Cameroon kusonga mbele bila wasiwasi kwenye hatua ya 16 bora ikiwa tayari na pointi 7 kwenye msimamo wa kundi A.

"Tumeongoza kundi letu jambo ambalo lilikuwa ndiyo lengo letu ingawa tulitamani tungeshinda mechi zote" amesema kocha wa timu ya taifa y Cameroon Toni Conceicao baada ya mchezo katika dimba la Olembe mjini Yaounde.

Burkina Fasso yailazimisha Ethiopia kukusanya virago 

Kamerun Bafoussam | Afrika-Cup | Burkina Faso v Äthiopien
Mshambuliaji wa Burkina Fasso, Cyrille Barros (kulia) akipongezwa na mwenzake wakati wa mchezo dhidi ya Ethiopia Picha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Hiyo Jumatatu pia kulikuwa na mchezo mwingine wa kundi A uliozikutanisha Burkina Fasso na Ethiopia katika mji wa Bafoussam kiasi kilometa 300 kutoka mji mkuu wa Cameroon, Yaounde.

Mchezo huo pia ulimalizika kwa ushindi tasa wa bao 1-1. Bao la Cyriller Bayala ndiyo iliiweka mbele timu hiyo dhidi ya Ethiopia na kuiwezesha kujiwekea nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano.

Ingawa Ethiopia ilifanikiwa kusawazisha kupitia goli la kiungo wake Getaneh Kebede lakini matokeo hayo hayakuweza kubadili hatma ya timu hiyo na kuilazimisha kufungasha virago kutoka michuano ya AFCON. Michezo ya kundi A  imemalizika kwa Ethiopia kuwa na pointi 1 pekee katika msimamo wa kundi hilo.

Katika kundi hilo ni Cape Verde yenye pointi 4 ndiyo inasubiri kuona kama itafanikiwa kupata nafasi ya bahati nasibu kusonga mbele kwenye hatua ya 16 bora.

Baadaye leo Jumanne michezo ya lala salama ya hatua ya makundi itaendelea. Malawi itakuwa na miadi na Senegal wakati Zimbabwe itakwaana na Guinea. Katika mchezo wa saa mbili usiku saa za Cameroon Gabon itakuwa inatoana jasho na Morroco.