1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani akutana na Condolezza Rice,Washington

4 Aprili 2006

Mawaizi wa mambo ya nje wa Ujerumani na Marekani wanakutana mjini Washington kujadili masuala kadhaa likiwemo suala la mgogoro wa mpango wa Nuklia wa Iran

https://p.dw.com/p/CBJB

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ambaye yupo nchini Marekani amekuwa na mazungumzo na maafisa wa Marekani juu ya mzozo wa mpango wa Nuklia wa Iran pamoja na suala la Mashariki ya kati.

Waziri huyo leo atakutana na mwenzake wa Marekani Condolezza Rice.

Bwana Steinmeir amekuwa na mazungumzo na mkuu wa usalama wa kitaifa wa Marekani Stephen Hadley pamoja na viongozi wengine wa baraza la wawakilishi la Marekani kabla ya kukutana leo hii na kiongozi wa masenata waliowengi bungeni Bill Frist na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezza Rice.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Scott McClellan amesema rais Gorge Bush alimpigia simu kansela wa Ujerumani Angela Merkel hapo jana kumueleza juu ya masuala ya Iran,Belarus,ziara ya bibi Rice nchini Iraq pamoja na masuala mengine.

Ziara ya siku mbili ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Steinmeir mjini Washington inanuiwa kutoa njia kwa ziara ya kansela Merkel nchini Marekani mnamo mwezi wa Mei.

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani,Martin Jaeger, Steinmeir na Hadley wamezungumzia hapo jana masuala yanayohusu Iraq,Iran,Ukraine,mtazamo wa mataifa ya magharibi kuelekea kundi la Hamas nchini Palestina kufuatia ushindi wake mkubwa kwenye uchaguzi wa bunge pamoja na mpango wa kihistoria wa Kinuklia baina ya Marekani na India.

Wiki iliyopita waziri Steinmeir aliukosoa mpango huo wa Kinuklia ambapo Marekani ilikubali kutoa technologia ya kinuklia kwa India ili India nayo itenganishe mipango yake ya atomi inayotumika kwa matumizi ya kiraia na ile ya Kijeshi.Steinmeir aliisema hatua hiyo ya Marekani haitosaidia kitu hasa katika mgogoro na Iran juu ya mpango wake wa Kinuklia.

Mazungumzo ya bibi Condolezza Rice na waziri Steinmeir leo hii yatatuwama kwenye mgogoro huo wa Iran juu ya mpango wake wa kinuklia,uchaguzi wa hivi karibu nchini Israel,msaada kwa serikali ya Palestina baada ya ushindi wa kundi la Hamas,Belarus na eneo la Balkans.

Mkutano huu pia unatarajiwa kuzungumzia uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali za Washington na Tehran.Wapatanishi wa Ulaya wameelezea matumaini kwamba mazungumzo baina ya Marekani na Iran huenda yakaleta mwafaka katika juhudi za kuishawishi Iran iachane na mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium,mpango ambao nchi za magharibi zinahofia huenda ukatumiwa kutengeneza bomu la atomiki.

Bibi Condolezza Rice alhamisi iliyopita alikuwepo mjini Berlin na kukutana na wanachama wengine wa nchi zenye uwezo mkubwa duniani na wanachama wakudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuzungumzia suala hilo la mgogoro wa Iran.

Mawaziri wa Uingereza,China,Urussi, Ufaransa,Marekani,pamoja na Ujerumani walijadili mikakati ya baadae iwapo Iran itashindwa kusitisha mpango wa ke wa Kinuklia. Mkutano huo wa mjini Berlin ulikuja siku moja baada ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kupitisha tamko la kuitaka Iran kukomesha mipango yake yote ya kurutubisha madini ya Uranium katika muda wa siku 30.