1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Waziri wa mambo ya nje wa Libya asimamishwa kazi

28 Agosti 2023

Kiongozi wa serikali ya Libya amesema kuwa amemsimamisha kazi waziri wake wa mambo ya nje baada ya mwenzake wa Israel kutangaza kuwa, wawili hao walifanya mazungumzo mjini Rome wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4VdGe
Waziri wa mambo ya nje wa Libya Najla Mangoush
Waziri wa mambo ya nje wa Libya Najla MangoushPicha: Jaber Abdulkhaleg/AA/picture alliance

Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah amesema jana jioni katika taarifa iliyochapishwa pia kwenye mtandao wa Facebook kuwa Najla al-Mangoush "amesimamishwa kazi kwa muda" na atakuwa chini ya uchunguzi wa tume inayoongozwa na waziri wa sheria.

Wizara ya mambo ya nje ya Libya imeelezea kuwa "mkutano huo ulikuwa sio rasmi na kwamba wawili hao walipatana tu bila kupanga," japo taarifa za mkutano huo tayari zimesababisha maandamano katika miji kadhaa ya Libya.

Mzozo huo wa kisiasa ulizuka jana baada ya wizara ya mambo ya nje ya Israel kueleza kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa Israel na Misri walikutana wiki iliyopita.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen na Mangoush, mwenzake wa Libya, walizungumza mjini Rome katika mkutano ulioandaliwa na Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani.

Israel imeuelezea mkutano huo kama mpango wa kwanza wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Tangu mnamo mwaka 2020, Israel imekuwa ikijaribu kurejesha uhusiano wake na mataifa kadhaa ya Kiislamu kupitia mkataba maarufu kama Abraham Accords, uliosimamiwa na Marekani.