1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Iran ajiuzulu.

26 Februari 2019

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, aliyeongoza mazungumzo ya kufikiwa kwa makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa mengine matano yenye nguvu duniani amejiuzulu ghafla.

https://p.dw.com/p/3E6WP
Deutschland München MSC Mohammed Dschawad Sarif
Picha: AFP/C. Stache

Zarif ametangaza kujiuzulu na kuliomba radhi taifa kwa kuchukua hatua hiyo ghafla. 

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif, aliandika taarifa ya kujiuzulu kupitia ukurasa wake wa twitter jana usiku. Shirika la habari la DPA, hii leo limearifu kwamba pamoja na rais Rouhani mapema hii leo kuthibitisha kujiuzulu kwa waziri Zarif, lakini limesema hatakubaliana na ombi hilo.

Miito imeongezeka kwa rais Rouhani kutoka kwa wabunge wa Iran na wenye ushawishi mkubwa ya kulikataa ombi hilo la Zarif. Taarifa iliyoandikwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa ofisi ya rais imesema, Zarif hatakuwa peke yake, serikali itamuunga mkono

Zarif mwenye miaka 59, ameitumikia wizara hiyo ya mambo ya nje tangu Agosti 2013, na katika kipindi hicho amekuwa akikabiliwa na shinikizo la mara kwa mara kutoka kwa wanasiasa wenye mrengo mkali wanaoipinga sera yake ya kuelegeza misimamo ya kimahusiano na mataifa ya Magharibi.

Sababu ya kujiuzulu kwake imeibua mjadala mzito kwenye majukwaa ya kijamii, huku baadhi wakidai amechoshwa na ukosoaji kutoka kwa wenye misimamo mikali, kuhusiana na mkataba huo wa nyukliapamoja na sera yake hiyo kuelekea mataifa ya magharibi.

Syriens Machthaber Bashar Assad besucht Ayatollah Ali Khamenei, den Führer der Islamischen Republik Iran
Rais Bashar al-Assad alipokutana na kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Khamenei jana Picha: Leader.ir

Wengine wanadai ameghadhibishwa na namna alivyowekwa pembeni katika mkutano na rais wa Syria, Bashar al-Assad jana Jumatatu. Kwa ujumla wanakubaliana kwamba kujiuzulu kwake huenda kukamaanisha kumalizika kwa haraka kwa makubalino hayo ya nyuklia, yaliyowezesha Iran kuondolewa vikwazo, ambayo hata hivyo tayari yalikumbwa na pigo baada ya Marekani kujiondoa mwaka jana.

Mataifa ya nje yazungumzia uamuzi wa Zarif.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuhusu hatua hiyo. Amesema Marekani imeipokea  na itaangalia iwapo itadumu. Amesema wanajua Khamenei atafanya maamuzi ya mwisho, na sera yao haibadiliki.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu nae ameandika kwenye twitter kuhusu hatua hiyo akisema ni uamuzi mzuri. Ameandika Zarif ameondoka na kuongeza kuwa, kwa kuwa bado mamlakani, Iran kamwe haitaweza kuwa na silaha za nyuklia.

Waangalizi waliopo Tehran wanaamini kwamba Iran haitaweza kuziba pengo la Zarif na mtu mwenye misimamo, haiba na uzoefu kama wake, si naibu wake Abbas Araghchi ama Ali-Akbar Salehi, ambaye ni mkuu wa shirika la nyuklia la Iran.

Katika hatua nyingine, rais wa Syria Bashar al-Assad amefanya ziara yake ya kwanza ya umma kwa mshirika wake wa karibu zaidi Iran, tangu kulipoibuka vita vya Syria mwaka 2011. Assad amekutana na rais Rouhani pamoja na kiongozi wa juu nchini humo Ayatollah Khamenei.

Viongozi hao wamesifu na kueleeza kuridhishwa na hatua za kimakakati walizozifikia. Rais Rouhani amesema ushindi wa Syria ni ushindi kwa Iran na ulimwengu wa kiislamu kwa ujumla, huku akimuhakikishia Assad kuendelea kumsaidia kile kinachowezekana kufanikisha vita dhidi ya ugaidi na mchakato wa ujenzi wa taifa hilo.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/DPAE/RTRE

Mhariri: Sekione Kitojo