1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza aambukizwa virusi vya Corona

27 Machi 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameambukizwa virusi vya Corona, huku idadi ya maambukizi nchini Marekani ikiongezea na Uhispania nayo ikitangaza idadi kubwa ya vifo ndani ya masaa 24.

https://p.dw.com/p/3a9Fy
Großbritannien London | Coronavirus | Boris Johnson, Premierminister
Picha: picture-alliance/empics/PA Video

Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, kiongozi huyo aligundulika kuugua virusi vya corona baada ya kuonyesha dalili za mwanzo za virusi hivyo ama homa kali na kikohozi. Taarifa hiyo inasema kwa sasa amejitenga lakini bado anaendelea kuiongoza Uingereza kupata majibu ya kukabiliana na janga la virusi hivyo

Akizungumza kupitia njia ya Video Johson amewataka raia wa Uingereza kuondoa wasiwasi akisema yuko katika hali nzuri ya kuendelea na majukumu yake.

"Nafanya kazi kutoka nyumbani najitenga, na hicho ndicho kitu muhimu cha kufanya. Lakini musiwe na shaka, nashukuru teknolojia maana naweza kuendelea kuwasiliana na kundi langu kuongoza jitihada za kitaifa za kupambana na janga hili la virusi vya Corona," alisema Johnson.

Wiki kadhaa zilizopita Boris Johnson aliye na miaka 55 aliapa kuendelea kusalimiana na watu kwa mikono licha tahadhari iliyotolewa ya kutofanya hivyo kama njia moja ya kuzuwia maambukizi zaidi. Waziri Mkuu huyo wa Uingereza amekuwa kiongozi wa kwanza wa taifa kubwa kuugua ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Idadi ya walioambukizwa yaongezeka mara dufu

Coronavirus in Italien Pavia Patient auf Intensivstation
Wagonjwa wa COVID 19 wahudumiwa katika hospitali mmoja nchini Italia Picha: picture-alliance/AP/LaPresse/C. Furlan

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amejitenga tangu daktari wake alipoambukizwa virusi hivyo lakini majibu ya vipimo vyake yameonyesha kuwa hajaambukizwa. Mapema wiki hii Mwanamfalme Charles wa Uingereza pia aliripotiwa kuambukizwa virusi vya Corona. Waziri wa Afya wa Uingereza Matt Hancock hata yeye amethibitishwa kuambukizwa virusi hiyvo hii leo.

Visa vya watu walioambukizwa virusi vya Corona vinaendelea kupanda. Uingereza ina maambukizi mapya yaliofikia 11,658 huku Marekani ikiipiku China na dunia nzima kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walioambukizwa wanaofikia 85,755. Nchini uhispania wizara ya afya imeripoti vifo 769 ndani ya masaa 24.  Nchi hiyo imetangaza wafanyakazi wake wa afya 9,444 wameambukizwa virusi vya hivyo vya Corona. 

Hali imeendelea kuwa mbaya katika mataifa mengine kama Urusi Indonesia na Afrika Kusini, wote wamepitisha idadi ya watu 1000 walioambukizwa.

Huku hayo yakiarifiwa India imeanzisha mpango wake mkubwa wa kuwalisha wafanyakazi wake baada ya marufuku ya kutotoka nje kusababisha raia wake bilioni 1.3 kukosa kwenda kazini. Wakati watu wakiendelea kuhimizwa kubakia nyumbani kama tahadhari ya kuzuwia kuenea kwa virusi  vya Corona, nchini Pakistan baadhi ya waumini wa kiislamu wamekiuka amri hiyo na kumiminika misikitini kuhudhuria sala ya Ijumaa.

Mataifa kama Saudi Arabia, Misri Uturuki na Indonesia wengi walitekeleza swala hiyo majumbani mwao.

Vyanzo: afp,ap