1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa mpito Libya aonya uwezekano wa kuzuka vita

22 Februari 2022

Waziri Mkuu wa mpito wa Libya Abdelhamid Dbeibah ameonya kuwa kuteuliwa kwa serikali mpya ya mpito kunaweza kusababisha vita na machafuko kwenye nchi hiyo ambayo tayari imekumbwa na mzozo wa muongo mmoja. 

https://p.dw.com/p/47Qc9
Ägypten Kairo | Libyscher Premierminister Abdul Hamid Mohammed Dbeibah
Picha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Akiwahutubia wananchi wa Libya jana, Dbeibah amerudia kuuelezea msimamo wake kwamba atakabidhi madaraka tu kwa serikali iliyochaguliwa.

Katika hotuba yake iliyokuwa na kurasa nane, Dbeibah amelitaja neno ''vita'' mara nane na ameuita mpango wowote wa kuiweka madarakani serikali mpya ya mpito kama kichekesho, wa kizembe na usio na maana ambao unaweza kusababisha vita zaidi.

Uchaguzi wa bunge Juni 24

Dbeibah alikuwa akizungumzia juhudi zinazoendelea kufanywa na Baraza la Wawakilishi kuithibitisha serikali mpya inayoongozwa na waziri mkuu mteule, Fathi Bashagha. Dbeibah ametangaza mpango wa kufanyika uchaguzi wa wabunge Juni 24, ambao ni mwisho wa kipindi cha mchakato wa kisiasa kilichowekwa na Umoja wa Mataifa.

Dbeibah amependekeza mpango wenye vipengele vinne kwa uchaguzi wa bunge kwa wakati mmoja na kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba mwishoni mwa mwezi Juni.

Uchaguzi huo utafuatiwa na wa rais baada ya bunge jipya kuandaa katiba ya kudumu. Hata hivyo, hakutoa muda wa uchaguzi wa rais. "Tutaanza na uchaguzi wa wabunge, ndiyo wabunge. Uchaguzi wa rais utafanyika kwa mujibu wa katiba ya kudumu," alisisitiza Dbeibah.

Libyen | Fathi Bashagha kandidiert als Präsident
Waziri mkuu mteule wa Libya Fathi Bashagha, aliyechaguliwa na bunge hivi karibuniPicha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Libya ambayo tayari imegawanyika kati ya tawala zinazohasimiana za mashariki na magharibi, imejikuta ikiwa na mawaziri wakuu wawili hasimu mjini Tripoli, baada ya nchi hiyo kushindwa kuitisha uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba.

Mapema mwezi huu, bunge la mashariki lilimchagua Bashagha, waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwa waziri mkuu na kumtaka aunde serikali mpya ya mpito. Bashagha kutoka mji wa magharibi wa Misrata, anapaswa kuwasilisha baraza lake la mawaziri kwa Bunge wiki hii. Uteuzi wa Bashagha ulikuwa sehemu ya mwongozo wa kisiasa ambao unataka uchaguzi wa rais ufanyike katika kipindi cha miezi 14 ijayo.

Juhudi za Dbeibah zakwama

Dbeibah amesema amefanya mazungumzo na wapinzani wake ili kuepusha mkwamo uliopo, lakini juhudi zake zimeshindikana. Dbeibah anamshutumu mpinzani wake, Kamanda Khalifa Haftar kwa kuchochea machafuko ya kisiasa kwenye nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Awali uchaguzi wa urais ulipangwa kufanyika Desemba 24, lakini uliahirishwa kutokana na mzozo kati ya pande zinazohasimiana kuhusu sheria zinazosimamia uchaguzi huo na wagombea wa urais wenye utata. Wabunge wamesema kwamba mamlaka ya serikali ya Dbeibah yalikamilika Desemba 24.

Taifa hilo la Afrika Kaskazini limekumbwa na vita tangu vuguvugu la mapinduzi lililoungwa mkono na Jumuia ya Kujihami ya NATO kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.

 

(AP, AFP)