1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Libya anusurika kifo

10 Februari 2022

Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid al-Dbeibah amenusurika jaribio la kumuua baada ya gari lake kushambuliwa kwa risasi. Hayo yanaripotiwa wakati kukiwa na mzozo mkali kati ya makundi ya kisiasa juu ya udhibiti wa serikali.

https://p.dw.com/p/46naK
Libyen Premierminister Abdul Hamid Mohammed
Picha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Chanzo hicho kimesema tukio hilo limetokea wakati waziri mkuu Dbeibah akiwa tayari karudi nyumbani na kuelezea kuwa tukio hilo ni jaribio la wazi la kumuuwa na kwamba uchunguzi umeanzishwa, na kuongeza kuwa washambuliaji walifanikiwa kutoroka.

Picha zilizochapishwa baadaye na kituo cha runinga cha Al Jazeera zilionyesha kile kilichoaminika kuwa gari la Waziri Dbeibah, ambalo lilionekana kuwa na alama ya risasi kwenye kioo cha mbele na sehemu zingine. Hata hivyo Reuters haikuweza kuthibitisha picha hizo mara moja na haikuzungumza na mashahidi wengine wa tukio hilo.

soma zaidi: Libya: Spika wa Bunge asema muda wa serikali ya mpito umemalizika

Ikiwa itathibitishwa, jaribio la kumuua Dbeibah linaweza kuuchochea mzozo juu ya udhibiti wa Libya baada ya kauli yake ya kuwa atapuuza kura iliyopangwa Alhamisi (10.02.2022) na bunge lenye makao yake mashariki mwa nchi ili kumuondoa katika wadhifa wake.

Katika wiki za hivi karibuni, vikosi vya jeshi vimekuwa vikiwakusanya wapiganaji na vifaa zaidi katika mji mkuu, na hivyo kuongeza hofu ya kwamba mgogoro huo wa kisiasa unaweza kusababisha machafuko.

Pande zinazozozana zimekuwa zikigombea nafasi hiyo baada ya mchakato wa uchaguzi kusambaratika huku kukiwa na mizozo kuhusu kanuni na uhalali wa Dbeibah kugombea urais baada ya kuahidi kutogombea.

Libya bado ipo njia Panda

Schweiz Libysches Dialogforum in Genf
Picha: UNITED NATIONS/AFP

Bunge, ambalo liliunga mkono vikosi vya mashariki wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, limetangaza kuwa serikali ya umoja wa kitaifa ni batili na itapiga kura  kumteua waziri mkuu mpya ili kuunda serikali nyengine.

Mshauri wa Umoja wa Mataifa na Nchi za Magharibi nchini Libya amesema bado wanaendelea kuitambua serikali ya Umoja wa Kitaifa. Dbeibah alisema katika hotuba yake wiki hii kwamba atakabidhi madaraka baada ya uchaguzi na si vinginevyo.

"Hatutaliacha jukumu letu katika serikali, ambalo tuliahidi kwa wananchi hadi pale uchaguzi utakapofanyika. Pia, serikali ya umoja wa kitaifa itaendelea na kazi yake hadi madaraka yakabidhiwe kwa serikali iliyochaguliwa," alisema Dbeibah

soma zaidi:Dbeibah: Atoa wito wa katiba kupatikana kabla ya uchaguzi

Libya imekuwa na amani na utulivu mdogo tangu mwaka wa 2011 kulipozuka maandamano yalioungwa mkono na NATO dhidi ya Muammar Gaddafi, na baadaye nchi hiyo iligawanyika mwaka 2014 kati ya makundi mawili yanayozona, moja likiwa mashariki na jengine magharibi mwa nchi.

Dbeibah alitawazwa mwezi Machi kama mkuu wa kundi linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ilikusudiwa kuunganisha taasisi za nchi zilizogawanyika na kusimamia maandalizi ya uchaguzi mwezi Disemba kama sehemu ya mchakato wa amani.

Chanzo: RTRE