1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

101111 Griechenland Regierungskrise

10 Novemba 2011

Viongozi wa vyama vya siasa nchini Ugiriki wanakutana na Rais Karolos Papoulias katika jaribio jipya la uundaji wa serikali mpya ya mseto, ikiwa bado jina la mrithi wa George Papandreou halijawekwa wazi hadi sasa.

https://p.dw.com/p/138Bc
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou (kulia) akiwasili kwenye mazungumzo ya kuunda serikali.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou (kulia) akiwasili kwenye mazungumzo ya kuunda serikali.Picha: dapd

Waziri Mkuu anayeondoka madarakani, George Papandreou, kiongozi wa chama cha kihafidhina, Antonis Samaras na kiongozi wa chama kidogo kinachoelemea siasa za mrengo wa kulia, George Karatzaferis, wameanza mazungumzo yao na Rais Papolious katika kasri la rais huyo.

Kuvunjika kwa makubaliano ya jana ya kumchagua spika wa Bunge la Ugiriki, Filipos Petsalnikos, kuwa waziri mkuu yalirudisha matumaini mengine kwa makamo rais wa zamani wa Benki Kuu ya Ulaya, Lucas Papademos, kushikilia wadhifa huo.

Mabishano baina ya marafiki wa zamani waliogeuka mahasimu wa kisiasa, Waziri Mkuu Papandreou na Saramas, yanalaumiwa kuwa chanzo cha mkwamo huu wa wiki nzima sasa juu ya mrithi wa Papandreou.

"Katika suala hili muhimu kwa nchi na linalohitaji hasa uongozi wa kitaifa, Bwana Papandreou na Bwana Samaras wanaonekana kuleta mchezo. Nami nimekasirishwa sana na mchezo wao." Amesema mmoja wa washiriki wa mazungumzo ya leo, George Karatzaferis.

George Papandreou (kushoto), Rais Carolos Papoulias (kulia) na kiongozi wa upinzani Antonis Samaras kwenye ikulu ya Ugiriki.
George Papandreou (kushoto), Rais Carolos Papoulias (kulia) na kiongozi wa upinzani Antonis Samaras kwenye ikulu ya Ugiriki.Picha: dapd

Katika hotuba yake ya jana (09.11.2011) kwa taifa kupitia televisheni, Papandreou aliwahakikishia Wagiriki kwamba licha ya kuondoka madarakani, ana imani na hatua alizochukuwa akiwa waziri mkuu wao kwamba zitaweza hatimaye kuiokoa nchi yao. Aliwataka viongozi wenzake wa kisiasa pamoja na wananchi wa kawaida kutimiza wajibu wao kwa taifa.

"Leo kuna habari zinazoleta matumaini na utulivu wa nafsi za Wagiriki wote: Tulipoamua kutekeleza mpango wa tarehe 26 Oktoba wa Umoja wa Ulaya, si kwamba matatizo yetu yote yalimalizika, lakini dhamira yetu ilikuwa safi kabisa na kwa hivyo tutaweza tena kusimama kwa miguu yetu wenyewe." Alisema Papandreou kwenye hotuba ya jana kwa taifa.

Lakini hicho anachokiita Papandreou kuwa ni habari za matumaini na utulivu wa nafsi, bado hakikuonekana hivyo, bali kinyume chake. Kwani kilimaanisha kutekeleza masharti ya msaada wa Umoja wa Ulaya kama yalivyo. Miongoni mwao ni kupoteza kazi kwa wafanyakazi 30,000 wa sekta ya umma. Na bado juu ya yote, hatua hizo zimemaanisha kuanguka kwa serikali na kuundwa mpya, ambako hadi sasa hakujafanyika.

Mazungumzo ya leo baina ya viongozi hao watatu wa vyama vya kisiasa, Papandreou, Samaras na Karatzaferis, mbele ya Rais Papoulius, yanatarajiwa kutatua angalau moja ya tata zinazoitatiza sasa Ugiriki. Kuingizwa kwa Karatzaferis, ambaye chama chake ni kidogo, kumetajwa kuwa ni kuongeza vipande vya chungwa kwenye mgao, na hivyo kuongeza fursa za kufikia makubaliano ya haraka.

Ama kama atakuwa Papademos, ambaye mwanzo alishafutwa kwenye orodha au atarudishwa tena Petsalnikos, ambaye naye hadi jioni ya jana alishaondolewa uwezekano, au mwengine nje ya hawa wawili, mchana huu utaamua. Na yeyote kati yao, hata hivyo, atajikuta na jukumu lile lile analoliwacha Papandreou, kuikwamua nchi iliyokwama kiuchumi na kisiasa.

Mwandishi: Thomas Borman/SWR/Reuters
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdulrahman