1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu mpya wa Thailand aapishwa na kuahidi mabadiliko

23 Agosti 2023

Waziri Mkuu mpya wa Thailand ameapa kuleta miaka minne ya mabadiliko katika taifa hilo la kifalme wakati akila kiapo leo.

https://p.dw.com/p/4VVms
Thailand Srettha Thavisin
Waziri Mkuu mpya wa Thailand Srettha ThavisinPicha: Chalinee Thirasupa/REUTERS

Waziri Mkuu mpya wa Thailand ameapa kuleta miaka minne ya mabadiliko katika taifa hilo la kifalme wakati akila kiapo leo. Srettha Thavisin ameapishwa rasmi kuuongoza muungano tata unaojumuisha vyama vya kijeshi vinavyohusishwa na viongozi wa zamani walioongoza mapinduzi.

Uteuzi wa Thavisin wa chama cha Pheu Thai ambacho kilihusishwa kwa muda mrefu na bilionea waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra-- ulihitimisha miezi kadhaa ya mkwamo wa kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu wa Mei.

Waziri Mkuu huyo mpya amesema kipaumbele chake ni kuifanyia nchi mambo mazuri akiongeza kuwa ana imani miaka minne ijayo itakuwa miaka ya mabadiliko.

Akizungumza baada ya kukubali ridhaa ya kifalme, Srettha amesema serikali yake itafanya kazi kwa ajili ya kuleta furaha kwa wote na kuifanya Thailand kuwa nchi ya matumaini kwa kizazi cha vijana.

Waziri mkuu anayeondoka Prayut Chan-o-cha, mkuu wa zamani wa jeshi aliyeipindua serikali iliyopita ya chama cha Pheu Thai katika mapinduzi -- alimpongeza Srettha na kumtakia kheri.