1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazanzibari wanapiga kura katika uchaguzi wa marudio

20 Machi 2016

Wazanzibari wanapiga kura leo katika uchaguzi wa marudio wa urais. Hali ya usalama imeimarishwa wakati polisi na wanajeshi wakishika doria. Upinzani umesusia zoezi hilo ukisema ni kinyume cha sheria

https://p.dw.com/p/1IGUL
Tansania Wahlen
Picha: Reuters/E. Herman

Hali visiwani Zanzibar imekuwa tete tangu uchaguzi wa kwanza ulipofutwa Oktoba mwaka wa 2015. Mapema wiki hii, kulikuwa na ripoti za polisi kuwatia mbaroni watu. Chama cha upinzani cha Civic United Front – CUF kimeitaka serikali ya Rais John Pombe Magufuli kusitisha ukiukaji wa haki za binaadamu ili kudumisha amani visiwani Zanzibar.

Siku chache kabla ya uchaguzi wa leo, mwandishi wa habari wa DW Salma Said alitekwa katika mazingira yasiyoeleweka. Wanaharakati wa haki za binaadamu na jumuiya ya wanahabari Tanzania na Zanzibar wametoa wito wa kuachiliwa kwake maramoja.

Mkurugenzi wa haki za binaadamu wa CUF Pavu Juma Abdallah ameiambia DW kuwa hali visiwani humo inaendelea kuwa mbaya. “Watu wanapigwa, wanaumizwa na kuna ofisi za vyama ambazo zinashambuliwa na kuharibiwa”. Aliongeza Abdallah.

Seif Sharif Hamad
Kiongozi wa upinzani Seif Sharif HamadPicha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Humode Mohammed Haroub ni mmoja wa watu waliokamatwa na polisi. Anasema raia wamekuwa watulivu na kuwa ni vyombo vya dola vinavyowashambulia watu bila sababu yoyote ya msingi. “watu wengi, nikiwemo, wanasema hawatapiga kura leo. Sijui nia ya serikali, lakini viongozi wetu wanatuhimiza kusalia nyumbani ikiwa tungependa amani”.

Upinzani kususia

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar – ZEC iliufuta uchaguzi wa rais visiwani humo mnamo 25.10.2015 ikitaja “ukiukaji wa sheria za uchaguzi”. Hatua hiyo ilikuja baada ya mgombe wa CUF Seif Shariff Hamad kujitangaza mshindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa. Chama cha CUF kimesema hakitashiriki katika uchaguzi huo wa marudio kwa sababu zoezi hilo ni kinyume na katiba.

Katibu mkuu wa CUF wa Wete, Pemba Riziki Omar amewataka Wazanzibari wengine hususan wale wanoheshimu utawala wa sheria na demokrasia pia wasusie uchaguzi huo

Ali Mohammed Shein Zanzibar
Rais wa Zanzibar Ali Mohammed SheinPicha: DW/M. Khelef

Rais Magufuli anaunga mkono uchaguzi mpya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli aliunga mkono kurudiwa uchaguzi wa urais Zanzibar licha ya upinzani kusema utasusia na hofu ya jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi mpya huenda ukazusha machafuko.

Kuna wagombea wengine wa urais kutoka vyama vidogo wanaoshiriki katika zoezi hilo, lakini uchaguzi visiwani Zanzibar aghalabu huwa kinyang'anyiro kikali cha farasi wawili baina ya CUF na Chama cha Mapinduzi – CCM, ambacho kimetawala Tanzania bara kwa zaidi ya miongo mitano.

Said Ismail, mfuasi wa CCM anasema ana matumaini kuhusu uchaguzi huo na kuwa anafurahia kuhusu uwepo wa polisi, lakini ana wasiwasi kuhusu kipindi kitakachofuata baada ya hapo.

Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein wa chama tawala cha muda mrefu CCM anasalia madarakani hadi uchaguzi utakapoamua.

“polisi wanaweka doria saa za usiku, lakini nini kitafanyika baada ya uchaguzi? Ni vipi watu wataendelea kuishi kwa umoja, kusaidiana na kushirki katika mikusanyiko kama vile harusi na matanga?”

Mwandishi: Caro Robi/Eunice Wanjiru/DW
Mhariri: Bruce Amani