1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavulana wote 12 na kocha waondolewa pangoni Thailand

Sylvia Mwehozi
10 Julai 2018

Hatimaye wavulana wote 12 na kocha wao ambao walikwama pangoni huko kaskazini mwa Thailand wemeweza kuokolewa na kukamilisha operesheni ya uokoaji ambayo ilitikisa ulimwengu mzima. 

https://p.dw.com/p/319Y4
Bildergalerie Thailand Höhlenrettung
Picha: picture-alliance/dpa/Chiang Rai PR office

Jeshi la wanamaji la Thailand kwa kushirikiana na wapiga mbizi wa kigeni wamewaondoa wavulana wanne waliokuwa wamesalia pangoni pamoja na kocha wao mwenye miaka 25 mchana wa leo Jumanne kupitia njia nyembamba zilizojaa maji.

Katika ukurasa wa Facebook wa jeshi hilo, waliandika kwamba " vijana wote wa timu ya mpira ya nguruwe mwitu na kocha wao wameondolewa kutoka pangoni, wakiwa salama."

Wavulana hao 12 walio na umri wa kati ya miaka 12 na 16 pamoja na kocha wao waliingia katika pango la Tham Luang lililoko kwenye vilima kaskazini mwa Thailand mnamo Juni 23 baada ya kufanya mazoezi ya mpira na kujikuta wamekwama wakati mvua kubwa iliposababisha mafuriko.

Walikaa humo kwa siku tisa wakiwa wamekwama kwenye kiza hadi wapiga mbizi wawili wa Uingereza walipowapata, wakiwa wamekondeana lakini walijawa na tabasamu na kuonekana kuwa katika ari kubwa.

Thailand Rettungsaktion Tham Luang Höhle
Gari ya kubebea wagonjwa ikiondoka eneo la pangoni Thailand Picha: Reuters/S. Zeya

Mamlaka zilifikiria mawazo mbalimbali ya namna ya kuwaondoa ikiwa ni pamoja na kuchimba mashimo katika vilima au kusubiri miezi kadhaa hadi pale msimu wa mvua za masika utakapomalizika ili waweze kutoka wenyewe, ambapo mkuu wa timu ya uokozi wakati mmoja alisema kuna uwezekano operesheni hiyo ikashindikana.

Pamoja na kiwango cha Oksijeni kupungua hadi kiwango cha hatari katika eneo walimokuwa na mvua za masika kuhatarisha mafuriko zaidi, waokoaji waliamua kuchagua njia ya kuwaondoa kutumia wapiga mbizi ambao waliwasindikiza kupitia njia nyembamba.

Njia hiyo ilikuwa changamoto hata kwa wapiga mbizi wazoefu, na wavulana hao hawakuwa na hata chembe ya uzoefu wa kupiga mbizi lakini waokoaji waliwafunza namna ya kutumia maski na kuvuta hewa chini ya maji. Hofu kubwa ilikuwa ni kwamba wavulana hao wangepatwa na mshutuko wakati wakipiga mbizi hata kama wanasindikizwa na wapiga mbizi wazoefu.

Kifo cha mpiga mbizi wa zamani wa jeshi la wanamaji ambaye aliishiwa Oksijeni katika eneo lililofurika mafuriko siku ya Ijumaa, klizidisha hofu na hatari ya operesheni ya uokoaji. Watoto hao watasalia katika karantini hospitali hadi madaktari watakapokuwa na uhakika kwamba hawana maambukizi kutoka ndani ya pango.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Saumu Yusuf