1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Watu zaidi ya 50 wafariki katika ajali ya meli Kongo

3 Oktoba 2024

Maiti zaidi ya 20 zimeopolewa baada ya meli kupinduka kwenye ziwa kivu. Watu kadhaa bado hawajulikani walipo katika mkasa huo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo linalokabiliwa na miundombinu duni

https://p.dw.com/p/4lNV1
DR Kongo | Huduma ya afya kwa majeruhi.
Wahudumu wa afya wakihudumia majeruhi katika eneo la ajali.Picha: Ruth Alonga

Taarifa zinasema kuwa meli hiyo iliyokuwa imewabeba abiria zaidi ya 150  na mizigo ilizama muda mfupi kabla ya kuwasili katika bandari ya mjini Goma. Ilikuwa inatoka kwenye mji wa Minova katika jimbo jirani la kivu kusini .

kulingana na vyanzo vya ndani , meli hiyo kwa jina Merdy, ilipinduka kabla ya saa nne asubuhi kwenye ziwa Kivu katika eneo la umbali wa karibu meta 200 hadi kwenye soko kuu la kituku .

Watu wachache walionusurika wamefikishwa mjini Goma wakiwa katika hali mahututi na wengine walifariki muda mchate tu baada ya kufikishwa nchi kavu. Bahati ombeni ni mmoja wa watu walionusurika katika ajali hiyo mbaya anaeleza zaidi.

Soma pia:Boti yapinduka kwenye ziwa Kivu Mashariki mwa Kongo na kuua takriban watu 50

Mbali na abiria waliokuwemo, meli hiyo pia ilikuwa imebeba shehena ya chakula na vifaa vingine muhimu kutoka katika mji mdogo wa Minova jimboni kivu kusini.  

Ziwa kivu, ndilo limesalia kuwa njia pekee inayotumiwa kusafirisha bidhaa kwenda katika mji wa Goma, tangu kufungwa kwa barabara na wapiganaji wa kundi la M23 miezi michache iliyopita . 

Raia waliofika hapa kutafuta miili ya wapendwa wao wameelezea kusikitishwa na kile wanacho taja kama uzembe wa serikali hasa linapokuja swala la miundombinu.

Juhudi za kutafuta manusura zaendelea

Polisi hata hivyo , imeendelea na zoezi la utafutaji wa abiria waliokosekana na kukusanya habari ili kugundua chanzo cha ajali hiyo mbaya zaidi.

DR Kongo | Waomboöezaji
Mmoja wa waombolezaji aliepoteza mpendwa wake katika ajali ya meli ziwa Kivu.Picha: Ruth Alonga

Mamia ya watu wameketi kando na magari yanayowasili katika eneo hilo la mkasa kuchukuwa miili ya watu inayo pelekwa mochwari mjini Goma huku huzuni ikiwa imetawala eneo hili.

Odette Kahindo anamtafuta mjomba wake aliyesafiri ndani ya meli hiyo ameiambia DW kwamba kuna haja ya serikali kuimarisha miundombinu hasa mtandao wa barabara kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Soma pia:Zaidi ya watu 80 wamekufa kutokana na ajali ya boti Kongo
Miaka miwili iliyopita , watu wasiopungua 55 walifariki dunia wakati boti iliyojaza abiria kuliko uwezo wake ilipozama kwenye mto kongo katika jimbo la mongala kaskazini mwa DRC .