1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wawili wauawa Burundi kufuatia shambulizi la gruneti

20 Septemba 2021

Watu wawili waliuawa na wengine wanane walijeruhiwa Jumapili jioni baada ya mlipuko wa gruneti katika mgahawa mmoja mjini Gitega nchini Burundi.

https://p.dw.com/p/40ZX5
Picha ya maktaba
Picha ya maktabaPicha: picture-alliance/AP Photo

Shirika la habari la AFP limeripoti tukio hilo kwa kunukuu vyanzo vya polisi leo Jumatatu. Shambulio hili linakuja siku mbili baada ya kundi la waasi la Red Tabara kunadi kuwa liliendesha mashambulizi mengine katika uwanja wa ndege wa mjini Bujumbura siku ya jumamosi. 

"Mlipuko huo wa gruneti dhidi ya baa moja katika mji wa Gitega ulisababisha uharibifu mkubwa, watu wawili waliuawa papo hapo na wengine wanane waliojeruhiwa walipewa matibabu katika vituo kadhaa vya afya mkoani Gitega," afisa mmoja wa polisi ambae hakutaka jina lake litajwe aliliambia shirika la habari la AFP.

Kulingana na chanzo cha afisa mwengine wa usalama, mgahawa huo unamilikiwa na afisa wa polisi na ni sehemu ambayo maafisa wengi na wanachama wa chama tawala nchini Burundi CNDD FDD hukusanyika.

Shambulio hili limethibitishwa pia na mashuhuda wawili waliotaja kuwa, watu zaidi ya kumi walijeruhiwa na kuwahishwa katika hospitali za mjii huo wa Gitega ambao ni makao makuu ya shughuli za kisiasa. Kwa wakati huo, haikuwezekana mara moja kuwatambua washambuliaji.

Hakuna kiongozi wa serikali ya Burundi alietaka kuzungumzia hadharani matukio haya mawili kuku vyombo vya habari vya ndani vikiamriwa kutoyazungumza.

"Mashambulio yote haya yamefanywa na maadui wa amani kwa lengo la kuonyesha kuwa kuna ukosefu wa usalama nchini Burundi wakati ambapo Mheshimiwa Rais Evariste Ndayishimiye alikua akielekea New York, Marekani katika ziara yake kubwa tangu achaguliwe kuiongoza Burundi.

Lakini hawatofikia chochote kwa sababu hali imedhibitiwa kikamilifu."Aliiambia AFP afisa mmoja mwandamizi katika serikali na ambae pia hakutaka jina lake litajwe.

Jumamosi jioni, siku moja kabla ya rais Ndayishimiye kuondoka kwenda New York, ambako atashiriki vikao vya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kundi la waasi la RED-Tabara lilifanya shambulio kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior Ndadaye huko Bujumbura.

Risasi zilizoskika hadi katikati mwa jiji, hazikusababisha uharibifu wowote na shughuli katika uwanja huo ziliendelea kama kawaida.

Kundi la RED-Tabara lililoibuka miaka 10 iliyopita na lenye misingi yake Kivu-kusini nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, ni miongoni mwa makundi ya waasi wa Burundi yanayotuhumiwa kuhusika katika mashambulio mabaya nchini humo tangu mwaka 2015.

(AFP)

Mwandishi: Bakari Ubena

Mhariri:Yusuf Saumu