1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watano wafariki baada ya mashua yao kuzama Ziwa Victoria

22 Machi 2021

Watu watano wamekufa baada ya mashua yao kuzama katika Ziwa Victoria umbali wa mita hamsini kutoka ufuo wa Arongo, katika mji wa Magharibi wa Kisumu nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/3qxOF
Bootsunglück auf dem Lake Viktoria in Uganda
Picha: Reuters

Naibu kaunti kamishna wa Kombewa, Biden Muchira, amesema tukio hilo lilitokea Jumamosi jioni baada ya mmoja wa abiria, kusimama ili kujipiga picha maarufu kama 'selfie' hali inayokisiwa kuweka uzito upande mmoja wa mashua hiyo kabla ya kuyumba na kuzama.

Juhudi za wavuvi na maafisa kutoka kitengo cha usalama wa majini waliokuwa karibu kutoa msaada zilifanikiwa kuwaokoa abiria watatu kati ya wanane huku juhudi za kuitafuta miili iliyozama zikifanikiwa kuopoa miili ya abiria watatu, miili mingine miwili ikiopolewa jana jioni.

Kaimu chifu wa eneo hilo, Shadrack Ocholla anasema tukio hilo lilijiri majira ya saa kumi na moja jioni Jumamosi na wanne kati ya watano waliofariki walikuwa waombolezaji waliomsindikiza mfanyakazi mwenzao kutoka Nairobi siku ya Ijumaa kuhudhuria mazishi kijijini.