1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 20 nchini Ethiopia wanakabiliwa na baa la njaa

12 Mei 2022

Watu milioni 20 wa jamii ya wachungaji nchini Ethiopia wanaelekea kuathirika vibaya kwa baa la njaa mwaka huu kutokana na kukosekana kwa mvua kwa mwaka mzima na nusu, kwa mujibu wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/4BB6I
Äthiopien | Folgen von Dürre - Totes Vieh
Picha: Hamar Woreda Government Communication Affairs Office

Kwa zaidi ya miezi 18 sasa, hakuna hata tone moja la mvua lililodondoka kwenye mkoa unaokaliwa na jamii ya Wasomali kusini mashariki mwa Ethiopia, ambako maiti za mbuzi, ng'ombe na punde imezagaa karibu na vibanda vya wanavijiji.

Umoja wa Mataifa unasema ukame huu unawafanya watu milioni 20 kwenye Pembe ya Afrika wawe kwenye ukingo wa kuangukia katika baa la njaa, unauharibu kabisa mfumo wa kale wa maisha, unaleta utapiamlo kwa watoto wadogo na unazipasuwa familia vipande vipande.

Soma pia: Afrika Magharibi katika hatari mbaya ya ukosefu wa chakula

Kawaida mwezi Aprili huwa moja ya miezi yenye mvua nyingi kwenye eneo hilo, lakini hadi sasa hali ya hewa ya Hargududo ni ya joto kali na kavu na ardhi ni vumbi tupu. Wanyama wengi wanaomilikiwa na familia 200 za wachungaji wameshakufa.

Hussein Habil, mwanakijiji mwenye umri wa miaka 52 ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu waliokuwa na mbuzi 300 kabla ya ukame, hivi sasa wamebakiwa na 50 ama 60 tu. Kwa wengine, hata mmoja hakubakia.

Ukame umeathiri maeneo ya kusini mwa Ethiopia, Kenya na Somalia.

Dürre in Somali Region
Wakaazi katika wilaya ya Adadle wakijaribu kuwaokoa mifugo iliyoathirika na ukame.Picha: Michael Tewelde/World Food Programme/REUTERS

Hali hii mbaya inayaathiri maeneo makubwa ya kusini mwa Ethiopia na katika mataifa ya jirani, Kenya na Somalia. Lakini nchini Ethiopia, macho ya walimwengu yameuelekea zaidi kwenye mzozo wa kibinaadamu uliosababishwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na vile vya Jeshi la Ukombozi la Watu wa Tigray, TPLF, ambao umewageuza watu milioni tisa wategemezi wa msaada wa dharura wa chakula.

Lakini Ofisi ya Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, inakisia kuwa watu milioni 6.5 nchini Ethiopia, ambao ni zaidi ya asilimia sita ya raia wote, wana pia shida kubwa ya chakula kutokana na ukame.

Ukosefu wa mvua umeuwa mifugo milioni 1.5 na sehemu kubwa ni kwenye mkoa wa Somalia nchini Ethiopia, kwa mujibu wa OCHA. Mifugo ndiyo chanzo kikuu cha chakula, fedha na akiba kwa watu wa jamii hiyo. Lakini hata wanyama waliosalia hai, hali zao zimedhoofika sana kiasi cha kupoteza thamani yao na hivyo kuufanya uwezo wa familia kukidhi mahitaji yao kushuka, kwa mjibu wa OCHA.

Soma pia: Ukame Pembe ya Afrika wasababisha njaa kwa watu milioni 13

Tarik Muhammad mwenye umri wa miaka 50 anasema kabla ya ukame kuanza, walikuwa wakitegemea wanyama wao kwa chakula, maziwa, na fedha, lakini sasa wengi wao wamekaa tu kijijini wakiwa hawana cha kufanya maana hakuna mifugo ya kuchungwa.

Ukame watishia mifugo na kilimo nchini Kenya

Jamii nzima hapa inasambaratika kwani kupoteza mifugo kunatishia mfumo wao wa maisha wa jamii ya wachungaji: wanavijiji wanalazimika kukimbia makaazi yao na kwenda kusaka kazi mjini, familia zinagawanyika, watoto wanapuuzwa wakati wazazi wao wakijaribu kuokowa mifugo yao, ambayo ni muhimu kwa maisha yao.

Kwa uchungu, Muhammad anasema. "Mfumo wetu wa maisha ya wachungaji umekufa!" Awali mfumo wa maisha wa jamii ya wachungaji ulikuwa unaamuliwa na mpishano wa miezi ya jua kali na mvua kubwa baina ya Machi na Aprili na Juni na Agosti. Hili lililifanya eneo hilo kuwa na majani takribani kwa muda wote. Lakini mara hii hakukuwa na mvua kwenye miongo mitatu mfululizo na msimu wa mwezi Machi nao pia ulimalizika bila ya dalili yoyote ya mvua kunyesha.

Zamani vipindi kama hivi vya ukame vilikuwa vikija kila baada ya miaka kumi, lakini sasa vinakuja mara kwa mara tafauti na awali, anasema Nur Mohamed kutoka shirika la misaada la Uingereza, Save the Children.