1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 700 wameuwawa na polisi Kenya

28 Desemba 2020

Zaidi ya watu 700 wamekufa wakiwa mikononi mwa maafisa wa polisi nchini Kenya tangu mwaka 2007. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/3nIBy
Kenia - erneute Proteste in Nairobi
Picha: picture-alliance/AA/B. Jaybee

Hata hivyo, msemaji wa polisi nchini humo Charles Owino amekanusha ripoti hiyo akisema kuwa maafisa wa polisi huzingatia sheria wanapotekeleza majukumu yao.

Takwimu kwenye tovuti la Shirka la Kutetea Haki za Binadamu la Missing Voices, linaloijumuisha Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya, zinaonesha kuwa mauaji yaliyotekelezwa na polisi mwaka 2020 ni ya pili yakilinganishwa na kipindi cha ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007. Ripoti hiyo inaeleza kuwa watu 144 waliuawa na maafisa wa polisi mwaka huu.

Inasemekana kuwa asilimia 59 ya mauaji hayo yalitokana na polisi kuwaua washukiwa kwa kuwapiga risasi. Mauaji mengine yalitokana na mateso na kurushiwa mabomu ya machozi.

Kufikia Juni watu 15 walikufa mikononi mwa polisi

Baadhi ya vifo hivyo vilitokea wakati polisi walipokuwa wakitekeleza amri ya kutotoka majumbani. Hata hivyo, msemaji wa polisi Charles Owino amesema mauaji yaliyotokea yalifanyika kwa bahati mbaya wala hayakukusudiwa.

Kenia Ausschreitungen Opposition Anhänger Odinga
Polisi wakikabiliana na raia KenyaPicha: picture-alliance/AP/B. Inganga

"Siwezi kusema kwamba kuna ukatili hivyo, lakini kitu cha kwanza na muhimu ni kuwa ni aibu kubwa sana kati yetu na wananchi, tunapokubaliana kwamba ikifika saa fulani kuna marufuku ya watu kutoka nje, lakini watu wanajifungia kwenye vilabu, sisi wenyewe hatuwezi kuvunja sheria,” alisema Owino.

Ripoti hiyo inasema kuwa kufikia Juni mwaka huu watu 15 walifia mikononi mwa polisi walipokuwa wakitekeleza sheria ya kutotoka majumbani. Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendajikazi wa Polisi, ilisema kuwa mwezi huo, ilikuwa imepokea malalamiko 87 dhidi ya polisi tangu kuanza kutekelezwa kwa sheria ya kutotoka majumbani iliyolenga kupunguza maambukizi ya visa vya COViD-19.

Polisi huhamishwa na kupelekwa kufanya kazi kwengine wanapopatikana na makosa

Malalamiko hayo yalikuwa ni pamoja na mauaji, mateso, wizi wa mabavu na dhulma. Otsieno Namwaya ni Mtafiti Mkuu katika Shirika la Human Rights Watch.

Demonstration in Nairobi nach Tod von Menschenrechtsaktivistin Caroline Mwatha
Baadhi ya waandamanaji wakiwa chini ya ulinzi wa polisiPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

''Kenya Human Rights Watch tumekuwa tukisema maafisa wa polisi wanaotumia nguvu kupita kiasi wachukuliwe hatua za kisheria, lakini serikali haijatuunga mkono. Wapelekwe mahakamani, wafutwe kazi na uchunguzi ufanywe kubaini ni kwa nini wanatumia nguvu kupita kiasi,'' alisema Otsieno Nyamwaya.

Mara nyingi polisi wanaopatikana na makosa nchini Kenya huhamishiwa kufanya kazi katika maeneo mengine, suala ambalo Otsieno anasema ni ukiukaji wa sheria na haki za binadamu.

Hayo yanajiri huku kisa cha hivi punde cha utumiaji wa nguvu kupita kiasi kikifanyika katika jimbo la Nakuru ambapo Mercy Cherono, msichana wa miaka 26 alipigwa na kujeruhiwa vibaya na polisi kwa madai ya wizi. Cherono alifungwa kwenye pikipiki na kuburutwa kwa mita mia mbili. Familia yake sasa inasema inataka kuona haki ikitendeka na maafisa husika washtakiwe kwa mujibu wa sheria.