1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaIndia

Watu 54 wapoteza maisha India kwa kunywa pombe yenye sumu

Sylvia Mwehozi
22 Juni 2024

Maafisa wa serikali nchini India wameeleza kuwa, watu 54 wamekufa baada ya kunywa pombe inayoaminika kuongezwa kemikali ya sumu katika jimbo la kusini la Tamil Nadu huku watu wengine zaidi ya 100 wamelazwa hospitali.

https://p.dw.com/p/4hNt1
Pombe za kienyeji India
Watu wengi wasio na kipato nchini India hunywa pombe zilizotengenezwa kienyeji ambazo usalama wake unatiliwa mashaka.Picha: picture alliance/dpa

Takribani watu 200 wanatibiwa tangu siku ya Jumatano kutokana na kutapika, kuharisha na kuumwa tumbo baada ya kunywa pombe inayoaminika kuongezwa kemikali ya metani katika wilaya ya Kallakurichi, karibu kilometa 250 kutoka mji mkuu wa jimbo la Tamil Nadu wa Chenai.

Serikali ya jimbo hilo ilisema kuwa imechukua hatua kubaini wale waliohusika na utengenezaji wa metani, kemikali yenye sumu ambayo kawaida hutumika viwandani.

Polisi wanachunguza tukio hilo na wanawashikilia watu 7 hadi kufikia sasa. Vifo vitokanavyo na unywaji wa pombe zinazozalishwa kienyeji nchini India, hutokea mara kwa mara ambako ni watu wachache wanaoweza kumudu pombe za viwandani.