1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 5 wajeruhiwa Afghanistan

MjahidA22 Februari 2012

Watu watano wameuwawa na wengine kujeruhiwa wakati wa maandamano katika mji wa Jalalabad mashariki mwa Afghanistan. Polisi waliwavyatulia risasi waandamanaji wanaopinga kuchomwa kwa nakala za Qoran, na majeshi ya Nato.

https://p.dw.com/p/147QE
Mmoja wa waandamanaji akionesha mabaki ya Koran iliochomwa
Mmoja wa waandamanaji akionesha mabaki ya Koran iliochomwaPicha: picture alliance/dpa

Waandamanaji mjini Kabul wamechoma moto ua la nyumba moja inayokaliwa na wageni, hii ikiwa ni siku ya pili ya maandamano baada ya nakala za kitabu kitakatifu cha Koran, kuchomwa moto katika kituo cha jumuiya ya Nato.

Kulingana na walioshuhudia, moto huo ulisambaa na kuteketeza eneo dogo la nyumba hiyo panapokaliwa wageni zaidi ya1500. Zaidi ya waandamanaji 26 walijeruhiwa katika kisa hicho.

Katika mji wa Jalalabad mashariki mwa Afghanistan, mtu mmoja ameuwawa na wengine kumi kujeruhiwa baada ya polisi kuwafyetulia risasi waandamanaji wanaopinga kuchomwa kwa nakala hizo za Qoran. Ahmad Ali said daktari katika hospitali ya eneo hilo amesema aliyeuwawa ni kijana mdogo huku akisema watu hao 10 waliopata majeraha ya risasi wanapata matibabu katika hospitali ya Jalalabad.

Kamanda wa kikosi cha Kimataifa cha kulinda amani Afghanistan ISAF John Allen.
Kamanda wa kikosi cha Kimataifa cha kulinda amani Afghanistan ISAF John Allen.Picha: AP

Kwa sasa polisi nchini humo wanajaribu kuwatawanya waandamanaji hao waliojawa na hamaki huku wakisema kwa sauti kuwa "kifo kwa Marekani".

Marekani yaomba msamaha.

Awali Marekani iliomba radhi kwa tukio hilo ikisema kwamba nakala hizo zilichomwa kwa bahati mbaya. Kamanda wa kikosi cha Kimataifa cha kulinda amani Afghanistan, ISAF, John Allen, amesema kamwe hawakukusudia kuchoma nakala hizo na si nia yao kuwaudhi waislamu kwa njia yoyote.

Leo mkuu wa polisi wa mjini Kabul, Mohammad Ayub Salangi, alifika katika eneo la maandamano na vikosi vyengine kadhaa ili kujaribu kuwatuliza waandamanaji. Daktari aliyezungumza na wanahabari lakini kwa njia ya siri amesema mtu mmoja aliyepigwa risasi yuko katika hali mbaya.

Kilometa kadhaa kutoka eneo la maandamano watu wengine walikusanyika karibu na kituo cha jeshi la Marekani na walikuwa wakirusha mawe. Baada ya tukio hilo la kuchomwa kwa Qoran kuwekwa wazi hapo jana zaidi ya waandamanaji 2,000 walimiminika barabarani wakipinga tukio hilo.

Mwandishi Amina Abubakar/AFPE/APE

Mhariri Josephat Charo