1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUgiriki

Ajali ya treni yasababisha vifo vya watu 32 Ugiriki

1 Machi 2023

Watu 32 wamekufa na wengine 85 kujeruhiwa nchini Ugiriki baada ya treni mbili kugongana. Maafisa wa serikali nchini humo wamesema kuwa huduma za dharura na uokoaji zinaendelezwa kuwatafuta manusura

https://p.dw.com/p/4O6Xr
Tschechische Republik | Zugunglück | Domazlice
Picha: Miroslav Chaloupka/AP/picture alliance

Gavana wa jimbo la Thessaly amesema kuwa treni ya kubeba abiria iliokuwa na abiria 350,  ilikuwa inaelekea katika mji  wa Kaskazini wa Thessaloniki kutoka Athens, ilipogongana kwa kasi ya juu na treni ya kubeba mizigo nje ya mji wa Larissa ulioko katika eneo la Kati mwa Ugiriki. Mabehewa kadhaa yalikaribia kuharibika kabisa huku gari moja likionekana kushika moto na kuwakwamisha ndani abiria wake. Moshi na ndimi za moto vilionekana kutoka kwa magari kadhaa baadhi ambayo yalikuwa yamepinduka yalipotoka kwenye njia kutokana na kishindo kikubwa na kuacha nyuma vioo na vyuma vilivyopasuka.

Treni ilikuwa imewabeba wanafunzi zaidi

Mmoja wa maafisa wa uokoaji aliyekuwa akitoka ndani ya mabaki hayo ya treni, alisema hajawahi kuona kitu kama hicho maishani mwake na kwamba baada ya masaa matano, wameanza kupata miili. Vyombo vya habari vya Ugiriki vimesema kuwa treni hiyo ilikuwa imewabeba wanafunzi wengi waliokuwa wakirejea Thessaloniki baada ya likizo ndefu ya mwisho wa juma.

Ajali ingeepukwa iwapo mifumo ya usalama ingefanya kazi.

Takis Theodorikakos - Neustart des Tourismus
Waziri wama mambo ya ndani wa Ugiriki Takis TheodorikakosPicha: ANE/picture alliance

Msemaji wa huduma za dharura za Ugiriki Vassilis Vathrakogiannis, amewaambia wanahabari kwamba maafisa 150 wa idara ya zima moto pamoja na magari 40 ya kubeba wagonjwa, yamepelekwa kusaidia katika juhudi hizo za uokoaji. Akiwa katika eneo la tukio hilo, rais wa chama cha madereva wa treni OSE Kostas Genidounias, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba treni hizo ziliishia kwenye njia moja na kugongana. Genidounias ameitaja ajali hiyo kuwa isiyofikirika na ingeepukwa iwapo mifumo ya usalama ingefanya kazi.

Mkutano wa dharura wafanyika baada ya ajali

Mkutano wa dharura wa serikali uliandaliwa baada ya ajali hiyo. Waziri wa Afya wa nchi hiyo Thanos Plevris alienda kwenye eneo la tukio, huku waziri wa mambo ya ndani Takis Theodorikakos akisimamia juhudi za uokoaji katika kituo cha kusimamia majanga. Hospitali mbili karibu na mji wa Larissa zimeombwa kuwapokea majeruhi wengi. Hii ni kulingna na idara ya zima moto huku hospitali za kijeshi katika miji ya Thessaloniki na Athens pia zikiwekwa katika hali ya tahadhari iwapo zitahitajika. Wakati huo huo, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na spika wa bunge la Ulaya  Roberta Metsola , wametoa risala zao za rambirambi kufuatia ajali hiyo na kusema Ulaya nzima inaomboleza na Ugiriki.