1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 15 wauwawa kwenye mapigano Somalia

Josephat Nyiro Charo29 Januari 2010

Wanamgambo wa al Shabaab washambulia wanajeshi wa kulinda amani

https://p.dw.com/p/LlR6
Maiti zikiwa zimezagaa katika kona ya barabara kusini mwa MogadishuPicha: AP

Mapigano makali yamezuka kati ya wanamgambo wa kisomali na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika mjini Mogadishu mapema leo. Duru zinasema watu wasiopungua 15 wameuwawa.

Mapigano mjini Mogadishu nchini Somalia yameanza upya leo alfajiri wakati wapiganaji wa kundi la al Shabaab walipoyashambulia majengo ya serikali na wanajeshi wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, AMISOM. Wanagambo hao baadaye wamerejea katika ngome yao kufuatia mapiganao hayo yanayoelezwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Somalia katika miezi kadhaa iliyopita.

Katika taarifa yake kundi la al Shabaab limedai kufanya harakati hiyo ya usiku wa kuamkia leo na kuwashutumu wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kwa kuwashambulia raia kwa mabomu. Kundi hilo pia limekiri kuwaua baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wakati wa operesheni yake mjini Mogadishu na kuapa kuendelea kuwashambulia wanajeshi hao. Maafisa wa tume ya amani ya Afrika nchini Somalia AMISOM, hawakupatikana kuweza kutoa taarifa kujibu madai hayo.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia mapigano hayo na duru za hospitali watu wengine takriban 25 wamejeruhiwa kwenye mapigano yaliyofanyika kwenye wilaya za Hodan Wardhigley na Howl Wadag mjini Mogadishu.

Akizungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la Reuters, waziri wa ulinzi wa Somalia, Sheikh Yusuf Mohammad Siad, ambaye ni mbabe wa kivita wa zamani, amesema vikosi vya serikali vimewaua wanamgambo zaidi ya 10 wakati wa mapigano ya usiku kucha. Amesema maiti zao bado zimezagaa katika maeneo kulikotokea mapigano. Waziri Siad amethibitisha kwamba hali ya wasiwasi imeongezeka sana mjini Mogadishu na raia wanaishi kwa hofu kubwa.

Uganda yalaumu jumuiya ya kimataifa

Uganda ambayo ina wanajeshi wake nchini Somalia imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali mjini Mogadishu. Waziri wa ulinzi wa Uganda,Crispus Kiyonga, ameilaumu jumuiya ya kimataifa kwa kutoupa kipaumbele mzozo wa Somalia ikilinganishwa na vita huko nchini Afghanistan au maeneo mengine ya mizozo duniani.

Naye msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulaije amesema kuna haja ya kuongeza wanajeshi zaidi wa kulinda amani nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji wanaotaka kuiangusha serikali ya nchi hiyo.

Wanamgambo wa al Shabaab wamefanya shambulio la leo kwa lengo la kuuvuruga mpango wa serikali ya Somalia pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kutaka kuudhibiti tena mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mwandishi: Charo, Josephat/Reuters/AFP

Mhariri: Miraji Othman