1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto kadhaa watekwa Nigeria

31 Mei 2021

Watu waliokuwa na silaha wamewateka takriban watoto 200 kutoka shule ya Kislamu kwenye jimbo la Niger nchini Nigeria. Hilo ni tukio la hivi karibuni miongoni mwa visa ambavyo vimekuwa vikiizonga. 

https://p.dw.com/p/3uDFU
Nigeria Abuja | Greenfield Universität | Entführte Studenten
Picha: Nasu Bori/AFP/Getty Images

Kupitia ukurasa wa Twitter, serikali ya jimbo hilo imesema takriban watoto 200 walikuwemo shuleni jana Jumapili wakati shambulizi hilo lilipotokea katika jimbo la Niger. Imeongeza kusema kwenye ujumbe huo kwamba watoto ambao idadi yao kamili haijulikani walitekwa.

Kisa hicho cha utekaji kimejiri siku 14 tu baada ya wanafunzi 14 wa chuo kikuu kimoja kilichoko kaskazini magharibi mwa Nigeria kuachiliwa huru baada ya kuwa mikononi mwa watekaji wao kwa siku 40.

Soma pia: Rais Buhari akabiliwa na shinikizo la ukosefu wa usalama

Msemaji wa polisi katika jimbo la Niger Wasiu Abiodun amesema watekaji hao waliwasili katika mji wa Tegina wakiwa kwenye pikipiki kisha wakaanza kufyatua risasi kiholela. Mkaazi mmoja aliuawa, na mwengine alijeruhiwa. Ndipo baadaye wakawateka wanafunzi wa shule ya Kiislamu ya Salihu Tanko.

Watekaji wawarudisha watoto wenye umri mdogo

Gavana wa jimbo hilo la Niger Wasiu Abiodun amewaagiza maafisa w ausalama kuhakikisha watoto waliotekwa wanarudishwa haraka iwezekanavyo
Gavana wa jimbo hilo la Niger Wasiu Abiodun amewaagiza maafisa w ausalama kuhakikisha watoto waliotekwa wanarudishwa haraka iwezekanavyoPicha: Nasu Bori/AFP/Getty Images

Afisa mmoja wa shule hiyo ambaye hakutaka kutambulishwa alisema awali washambuliaji waliwateka zaidi ya wanafunzi 100, lakini baadaye waliwarudisha baadhi yao waliokuwa na umri wa kati ya miaka minne na kumi na miwili wakisema walikuwa na umri mdogo sana kwao.

SOma pia: Utekaji Nigeria wafikia kiwango cha mzozo

Serikali ya jimbo hilo kupitia mfululizo wa jumbe kwenye mtandao wa Twitter imesema washambuliaji hao waliwaachilia wanafunzi 11 ambao walikuwa wadogo sana na hawakuweza kutembea muda mrefu.

Baadaye serikali hiyo ya jimbo iliandika tena ujumbe kwenye Twitter ikisema gavana wa jimbo hilo Sani Bello ameagiza vikosi vya usalama kuhakikisha wanafunzi hao wamerudishwa haraka iwezekanavyo.

Utekaji watu ili kuitisha kikomboleo

Mnamo Aprili, wanamgambo waliokuwa na bunduki walivamia chuo kikuu cha Greenfield kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuwateka wanafunzi 20.
Mnamo Aprili, wanamgambo waliokuwa na bunduki walivamia chuo kikuu cha Greenfield kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuwateka wanafunzi 20.Picha: Nasu Bori/AFP/Getty Images

Magenge yenye silaha yamekuwa yakiwahangaisha wakaazi wa Kaskazini magharibi na Eneo la kati la Nigeria kwa kupora mali vijijini, kuiba mifugo na kuwateka watu nyara. Utekaji nyara wa watu umekuwa mbinu inayotumiwa na wahalifu kujipatia fedha kwa kuitisha kikomboleo au fidia ili kuwaachilia walioshikwa mateka.

Kando na shambulizi la Jumapili, jumla ya watoto 730 miongoni mwao wanafunzi wametekwa tangu Disemba 2020. 

Mnamo Aprili, wanamgambo waliokuwa na bunduki walivamia chuo kikuu cha Greenfield kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuwateka wanafunzi 20. Aidha mfanyakazi mmoja wa chuo hicho aliuawa wakati wa tukio hilo.

Soma pia: Wanafunzi 279 waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru

Siku chache baadaye, wanafunzi watano miongoni mwa waliotekwa waliuawa kama njia ya kuwatia hofu wazazi wengine na serikali kulipa kikomboleo au fidia ndipo watoto waliosalia waachiliwe la sivyo wauawe pia. Kumi na wanne waliachiliwa huru siku ya Jumamosi. Vyombo vya habari katika jimbo hilo vimeeleza kwamba familia zililipa kikomboleo cha naira milioni 180, sawa na dola 440,000.

Utekaji umekithiri Nigeria?

Baadhi ya waandamanaji mjini Abuja May 4, 2021 wakitaka serikali kukomesha kabisa visa vya utekaji wa watu.
Baadhi ya waandamanaji mjini Abuja May 4, 2021 wakitaka serikali kukomesha kabisa visa vya utekaji wa watu. Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Kwa miaka mingi Nigeria ambayo ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika imekuwa ikizongwa na visa vya utekaji nyara huku wahalifu wakizilenga haswa familia tajiri na watu mashuhuri.

  Lakini katika miaka ya hivi karibuni, utekaji umetanuka hivi kwamba hata watu maskini wamekuwa wakitekwa na kulazimishwa kulipa kikomboleo.

Mapema mwezi huu, mamia ya waandamanaji waliziba barabara kuu kuingia mji mkuu Abuja, wakilalamikia misururu ya visa vva utekaji katika eneo hilo na kutaka vikomeshwe.

Magenge hayo ya uhalifu yamepiga kambi katika msitu wa Rugu ambao ukubwa wake unajumuisha pia majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna na Niger.

(AFPE, RTRE)