1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watano wafa kwa ugonjwa usiojulikana nchini Tanzania

17 Machi 2023

Tanzania imepeleka timu ya watalaamu wa afya kuchunguza ugonjwa usiojulikana ambao umesababisha vifo vya watu watano.

https://p.dw.com/p/4OpeG
Ebola virus in Uganda
Picha: ISAAC KASAMANI/EPA-EFE

Taarifa ya wizara ya afya imesema ugonjwa huo uligundulika katika jumla ya watu saba waliokuwa na dalili za homa, kutapika, kutokwa damu katika sehemu tofauti za mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Mganga mkuu wa serikali Dr Tumaini Nagu amesema serikali imetuma timu ya dharura katika eneo la Kagera ambalo linapakana na Uganda ili kuuchunguza ugonjwa huo wa kuambukiza

Uchunguzi huo unafuatia mripuko wa Ebola nchini Uganda, ambao ulidumu kwa miezi minne na kusababisha vifo vya watu 55 kabla ya serikali kutangaza Januari kuuangamiza mlipuko huo.

Tayari serikali imeamuru vijiji walikotoka wagonjwa hao kuwekwa katika uangalizi maalum na tahadhari mbalimbali zimetolewa kwa jamii ikiwemo kujiepusha kugusana mikono na kutowagusa watu wenye dalili za ugonjwa huo bila tahadhari.

Tansania Präsidentschaftswahl Nationalflagge
Tayari serikali ya Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi katika kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo.Picha: DW/M. Khelef

Ugonjwa huo ambao dalili zake zinashabihiana na dalili za ugonjwa wa Ebola ambao hivi karibuni uliripotiwa nchini Uganda, umesababisha taharuki kubwa kwa jamii nchini Tanzania hususani mkoa wa Kagera na maeneo yake ya jirani

Waliopoteza maisha ni pamoja na mtumishi mmoja wa zahanati ya Maruku mkoani Kagera ambaye anatajwa kuwa ndiye aliyemhudumia mgonjwa wa kwanza aliyefikishwa katika kituo hicho cha matibabu.

Tayari serikali imeamuru vijiji walikotoka wagonjwa hao kuwekwa katika uangalizi maalum na tahadhari mbalimbali zimetolewa kwa jamii ikiwemo kujiepusha kugusana mikono na kutowagusa watu wenye dalili za ugonjwa huo bila tahadhari

Mara kwa mara Tanzania imekuwa ikichukua tahadhari kubwa dhidi ya magonjwa ya mlipuko na ya kuambukiza ikiwemo kufanya ufuatiliaji ama upimaji kwa abiria wanaovuka mipaka ya Tanzania na nchi jirani