1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Azali Assoumani arejea madarakani baada ya ushindi

17 Januari 2024

Katika mji mkuu Moroni askari na wanajeshi wamemwagwa kukabiliana na maandamano ya upinzani unaotaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe

https://p.dw.com/p/4bNQs
Rais Azali Assoumani
Rais Azali Assoumani atangazwa mshindiPicha: REUTERS

Upinzani nchini Comoro umetaka matokeo ya uchaguzi wa rais yafutwe,huku hali ya wasiwasi ikitanda katika nchi hiyo ya visiwa.

Polisi walifyetuwa gesi ya kutowa machozi dhidi ya waandamanaji waliokasirishwa na hatua ya kurudi madarakani kwa rais Azali Assumani.

Azali Assoumani ametangazwa mshindi akitajwa kupata asilimia 62.97 ya kura baada ya uchaguzi wa Jumapili ingawa wagombea watano wa upinzani wanayapinga matokeo hayo wakidai udanganyifu ulifanyika .

Wapinzani wanadai masanduku ya kupiga kura yalijazwa kura hata kabla ya zoezi la uchaguzi .

Wapiga kura katika mji wa Moroni
Wananchi wa Comoro wakipiga kuraPicha: REUTERS

Katika mji mkuu Moroni waandamanaji walichoma moto matairi na kuzizuia barabara nyingi za mji huo mapema leo asubuhi baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi.

Katika taarifa yao ya pamoja wagombea wa upinzani waliyapinga matokeo wakisema hayana uhalali wowote na kwamba yanapaswa kufutiliwa mbali. Msemaji wa serikali Houmed Msaidie akizungumza na shirika la habari la AFP amewashutumu wapinzani kwa kuandaa maandamano hayo.

Amesema watu kadhaa wamekamatwa japo alikataa kutowa idadi ya waliokamatwa, lakini akaongeza kusema kwamba ni jambo la kawaida kabisa watu kukamatwa ikiwa kuna wanaotaka kuvuruga amani ya umma.

Askari wa kikosi maalum cha gendarmes na wanajeshi walimwaga kwa wingi kuanzia asubuhi na walitumia mabomu ya gesi ya kutowa machozi kuwatawanya wananchi waliomwagika mitaani na kuwalazimisha kurudi majumbani mwao.

Kituo cha kupiga kura Moroni
Wapiga kura waliokusanyika kwenye kituo cha upigaji kura MoroniPicha: Issihaka Mahafidhou/REUTERS

Katika wilaya ya Coulee inayokaliwa na watu wenye kipato Kaskazini mwa mji wa Moroni makundi ya vijana walivurumisha mawe wakiwalenga wanajeshi  japo wakaazi wengi walionekana kujiandaa kukimbia,wakikhofia juu ya kuzuka kwa mivutano zaidi. Mama mmoja aliyekataa kutajwa jina alisema hivi:

''Naogopa kila kitu kinachoendelea na hasa mabomu ya kutowa machozi na hii hali ya kuwepo askari kila mahala,sijazowea kuona yote haya inaogopesha sana. Sikuwa hata na amani nyumbani kwangu na sikupata hata namna ya kumfuata mwanangu shule. Na nilipopata nafasi kidogo nilitumia fursa hiyo kwenda kumfuata binti yangu.Nataka kwenda ambako hakuna wasiwasi.''

Bibi mwingine  kwa jina Amina ambaye anaduka katika soko lenye shughuli nyingi la Volovolo, alisikika akisema kila mmoja ameshakimbia nayeye anauhama mji.

Idadi ya waliojitokeza kupiga kura Jumapili ilikuwa ndogo mno,asilimia 16 tu na kwahivyo idadi kubwa iliyotajwa ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais na wa magavana imeibuwa maswali na mashaka.

Wagombea wa upinzani wanasema wameshangazwa na matokea rasmi yanayoonesha kwamba zaidi ya thuluthi tatu ya watu walipiga kura kuwachaguwa magavana lakini wapiga kura hao hao hawakupiga kura ya uchaguzi wa rais katika vituo hivyohivyo walivyopiga kura. Wapinzani wanasema kilichofanyika ni kiini macho kwasababu hilo ni suala haliwezekani.