1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Kifo cha bin Laden bado kuthibitishwa

25 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CD99

Saudi Arabia imesema hapo jana kwamba haina ushahidi kuwa Osama bin Laden amekufa na hiyo kuweka mashaka zaidi kwa waraka wa siri uliovuja nchini Ufaransa uliosema kwamba majasusi wa Saudi Arabia wanaamini kwamba amefariki mwezi uliopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Douste-Blazy amesema kwamba kwa kadri anavyofahamu kiongozi huyo wa Al Qaeda mzaliwa wa Saudi bado yuko hai.

Amekiambia kituo cha televisheni cha LCI kwamba kwa uwelewa wake Osama bin Laden hakufariki lakini ameongeza kusema kwamba hakuiona repoti hiyo ya siri ya shirika la ujasusi la Ufaransa iliochapishwa na gazeti ambayo imesema Saudi Arabia ilikuwa ina imani kwamba bin Laden amekufa kutokana na homa ya matumbo nchini Pakistan mwezi uliopita.

Ufaransa,Marekani na Uingereza zilisema hapo awali kwamba zilikuwa haziwezi kuthibitisha repoti hiyo.

Wakati huo huo katika mahojiano ya mvutano na kipindi cha televisheni cha Fox News Jumapili Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton ametetea hatua zake za kushughulikia tishio la bin Laden kwa kusema kwamba alijaribu kutaka bin Laden auwawe na alishambuliwa kwa jitihada zake hizo na watu hao hao ambao hivi sasa wanamshutumu kwa kutochukuwa hatua za kutosha.