1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Hakuna uhusiano wa Saddam na Al Qaeda

9 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDE6

Repoti iliyotolewa na baraza la Senate la bunge la Marekani limesema kwamba kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam Hussein hakuwa na uhusiano na kundi la Al Qaeda kabla ya vita vya Iraq akiwemo kiongozi aliyeuwawa Abu Musab al Zarqawi.

Tathmini hiyo inapingana na madai yaliotolewa na Rais George W Bush wa Marekani na maafisa wake wa karibu ambao wamesema kulikuwa na uhusiano wa wazi kati ya Saddam na kundi la Al Qaeda.

Repoti hiyo ambayo ni sehemu ya pili ya uchunguzi wa baraza la Senate kwa matukio ya kabla ya vita vya Iraq pia imesema kwamba Iraq ilikomesha mpango wa nuklea hapo mwaka 1991.

Mojawapo ya hoja kuu za utawala za Bush kuingia vitani ilikuwa chini ya msingi wa madai kwamba Iraq ilikuwa inamiliki silaha za maangamizi makubwa.