1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washambuliaji wauwa 50 kanisani Nigeria

6 Juni 2022

Watu wenye silaha wamelivamia kanisa moja la Kikatoliki kusini magharibi mwa Nigeria na kuwauwa watu wapatao 50 waliokuwa kwenye ibada, wakiwemo wanawake na watoto.

https://p.dw.com/p/4CKNU
Nigeria | Dutzende Tote bei Angriff auf Pfingst-Gottesdienst
Picha: Rahaman A Yusuf/AP/picture alliance

Msemaji wa polisi wa jimbo la Ondo, Ibukun Odunlami, alisema siku ya Jumapili (Juni 5) washambuliaji hao waliwamiminia risasi watu waliokuwapo nje na ndani ya jengo la kanisa, wakiuwauwa na kuwajeruhi wengine kadhaa. 

Ingawa msemaji huyo hakutaja idadi ya waliouawa ama kujeruhiwa katika Kanisa la Mtakatifu Francis kwenye mji wa Owo, lakini daktari mmoja kwenye hospitali ya Owo aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba miili ipatayo 50 imepelekwa kwenye hospitali mbili za mji huo kutokana na mashambulizi hayo. 

Daktari huyo, ambaye alikataa kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji rasmi, alielezea pia uhitaji mkubwa wa damu kwa ajili ya kuwatibu majeruhi.

Rais Muhammadu Buhari aliyalaani mashambulizi hayo, aliyoyaita kuwa ya kinyama, huku Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, akituma ujumbe wa sala kwa wale aliowaita "wahanga walioshambuliwa kikatili wakiwa kwenye sherehe."

"Mauaji ya maangamizi"

Nigeria | Dutzende Tote bei Angriff auf Pfingst-Gottesdienst
Watu wakiwa wamesimama nje ya Kanisa la Mtakatifu Francis mjini Owo, Nigeria, baada ya mauaji ya Jumapili, 5 Juni 2022.Picha: Rahaman A Yusuf/AP/picture alliance

Gavana wa jimbo  la Ondo, Arankurin Oluwatotimi Akeredolu, ambaye alilitembelea eneo la tukio na majeruhi walioko hospitalini, ameyaelezea mashambulizi hayo ya jana Jumapili kuwa ni "mauaji makubwa ya maangamizi", ambayo yasingewachwa kutokea tena.

"Ni jambo la kusikitisha kwamba wakati Misa Kuu inaendelea, watu wenye silaha wasiofahamika walilishambulia Kanisa la Mtakatifu Francis na sasa watu wengi wanakhofiwa kuuawa na kujeruhiwa na Kanisa kunajisiwa." Alisema msemaji wa Kanisa Katoliki nchini Nigeria, Padri Augustine Ikwu, aliyeongeza kuwa askofu mkuu pamoja na mapadri wengine wa parokia hiyo walisamilika bila kudhurika.

Washambuliaji hawajafahamika

Nigeria | Dutzende Tote bei Angriff auf Pfingst-Gottesdienst
Madhabahu ya Kanisa la Mtakatifu Francis baada ya mashambulizi kusini magharibi mwa Nigeria siku ya Jumapili, 5 Juni 2022.Picha: Rahaman A Yusuf/AP/picture alliance

Hadi sasa, lengo la mauaji hayo na walioyafanya hawajafahamika, lakini kwa miaka kadhaa sasa Nigeria imekuwa ikipabamana na uasi wa makundi yenye itikali kali upande wa kaskazini mashariki na majambazi wenye silaha wanaovamia na kuteka watu kwa ajili kudai fedha za kikomboleo, hasa upande wa kaskazini magharibi.

Lakini kwenye upande wa kusini magharibi, mashambulizikama haya huwa ya nadra sana.

Mashambulizi haya yamefanyika siku moja kabla ya kuanza kwa kura za mchujo za chama tawala cha APC kwa ajili ya kusaka mgombea wake atakayemrithi Muhammadu Buhari kwenye uchaguzi wa mwakani.

Kwa yeyote atakayeshinda uchaguzi huo, suala la usalama litasalia kuwa changamoto kubwa katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika na ambalo uchumi wake ni kati ya chumi kubwa za bara hilo.