1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wa Trump waungana kuonyesha mshikamano

17 Julai 2024

Wapinzani wakuu wa zamani wa Donald Trump Nikki Haley na Ron DeSantis wameunga mkono ugombea wake kwenye mkutano mkuu wa chama cha Republican katika hatua ya kuonyehsa mshikamano baada ya Trump kuponea jaribio la kuuawa.

https://p.dw.com/p/4iPrb
Nikki Haley, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa
Nikki Haley asema anamuunga mkono Donald Trump katika nia yake ya kuiongoza tena Marekani Picha: Paul Sancya/AP/picture alliance

Nikki Haley, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa mpinzani wa mwisho wa Trump katika uchaguzi wa mchujo wa Republican, aliwahutubia moja kwa moja wafuasi wake baada ya kupanda jukwani huku akishangiliwa na baadhi wengine wakimzomea.

Haley ambae alimuelezea Trump  kama mtu asiyefaa kuchaguliwa na asiyefaa kushika wadhifa huo wakati wa kampeni, aliwataka wafuasi wake kumpigia kura dhidi ya Rais Joe Biden kwa ajili ya taifa lao.

Trump apokelewa kwa shangwe na Waprepublican

"Donald Trump ana uungaji mkono wangu thabiti. Tukiwa na miaka minne zaidi ya Biden au hata siku moja tu ya Harris, nchi yetu itakuwa katika hali mbaya zaidi. Kwa ajili ya taifa letu, inabidi twende na Donald Trump," alisema Nikki Haley.

Uhusiano kati ya Haley, gavana wa zamani wa jimbo la South Carolina, na Trump uligeuka wa mashambulizi binafsi, huku Haley akihoji iwapo rais huyo wa zamani alikuwa sawa kiakili kugombea wadhifa huo, na Trump akimlenga Haley, binti wa wahamiaji wa Kihindi, kwa matamshi ya ubaguzi wa rangi.

Marekani haiwezi kumudu miaka mingine ya utawala wa Biden.

Ron DeSantis
Gavana wa Florida Ron DiSantisPicha: Tim Hynds/Sioux City Journal/AP/picture alliance

Wakati Haley na DeSantis, gavana wa Florida aliejiondoa baada ya kura ya mchujo jimboni Iowa mwezi Januari, wamemuidhinishe hadharani Trump tangu wakati huo, uungwaji mkono wao uliotolewa kwenye mkutano mkuu wa taifa unaonekana kama ishara ya umoja ndani ya Chama cha Republican.

Gavana wa Florida Ron DiSantis alisema Marekani haiwezi kumudu miaka mingine ya utawala wa Biden.

Rais Biden asema hatoacha kumkosoa Trump

"Maisha yalikuwa rahisi zaidi wakati Donald Trump alipokuwa rais. Mpaka wetu ulikuwa salama zaidi chini ya utawala wa Trump na nchi yetu iliheshimiwa wakati Donald Trump alipokuwa amiri jeshi mkuu wetu," alisema DiSantis. 

JD Vance kuhutubia katika mkutano wa Republican.

Donald Trump na JD Vance
mgombea mwenza wa Trump, JD Vance Picha: Gaelen Morse/REUTERS

Hii leo 17.07.2024 mgombea mwenza wa Trump, JD Vance atajitambulisha kwa hadhira ya kitaifa atakapohutubia mkutano huo kwa mara ya kwanza kama makamu wa rais mteule. Vance ni mtu asiefahamika sana kwenye nyanja ya siasa ambaye alibadilika katika miaka ya karibuni kutoka mkosoaji mkubwa wa Trump na kuwa mtetezi mkubwa.

Vance mwenye umri wa miaka 39 amewekwa katika nafasi ya kuwa kiongozi ajaye wa vuguvugu la rais huyo wa zamani, ambalo limeunda upya chama cha Republican na kuvunja taratibu nyingi za zamani za kisiasa. Vance anajiunga na kinyang'anyiro hicho katika wakati ambapo maswali yanaulizwa kuhusu umri wa wagombea wakuu wa vyama vyote viwili.

Trump amchagua Seneta JD Vance kama mgombea mwenza

Wakati huio, Rais Joe Biden anajaribu kufufua kampeni yake miongoni mwa wapiga kura waliokata tamaa ambao ni muhimu kwa nafasi yake ya kuchaguliwa tena anapokutana Jumatano na wanachama wa shirika la kutetea haki za kiraia la Walatino katika jimbo la Nevada.