1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Syria washindwa kuungana

Admin.WagnerD3 Julai 2012

Wapinzani wa serikali ya Syria wanajaribu kuunganisha juhudi zao katika mkutano unaowaleta pamoja katika mji mkuu wa Misri, Cairo, lakini mgawanyiko baina ya makundi tofauti yao bado unakwamisha juhudi hizo.

https://p.dw.com/p/15Qb2
Mkutano wa wapinzani wa Syria Mjini Cairo
Mkutano wa wapinzani wa Syria Mjini CairoPicha: Reuters

Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu vuguvugu la mageuzi lilipoanza nchini Syria, lakini bado makundi ya upinzani yanaghubikwa na mgawanyiko, ambao umezuia kuwepo kwa kikundi kimoja chenye sauti kubwa, ambacho kinaweza kuchukuliwa kama mbadala kwa serikali inayoongozwa na rais Bashar al Assad.

Mkutano wa Cairo unawaleta pamoja wajumbe zaidi ya 250 kutoka vikundi tofauti vya upinzani dhidi ya serikali ya Syria. Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Jumuiya ya Nchia za Kiarabu, Nabil Elaraby, amewahimiza wapinzani hao kutumia vizuri nafasi iliyopo kwa kuzingatia kuwa kujitolea kwa watu wa Syria kuna umuhimu kuliko tofauti zinazowagawa.

Naye Nasser al Kidwa, mjumbe wa mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro wa Syria, Koffi Annan, amewaambia wapinzani hao wa Syria kuwa kufikia msimamo wa pamoja ni kitu cha lazima ili kupata uungaji mkono wa raia wengi, na kujijengea heshima na uhalali machoni mwa jumuiya ya kimataifa.

Hakuna muafaka juu ya masuala ya msingi

Wapinzani 250 wameshiriki katika mkutano huo
Wapinzani 250 wameshiriki katika mkutano huoPicha: Reuters

Kiini cha mapinduzi ndicho chanzo kikubwa cha mgawanyiko baina ya wapinzani wa Rais Bashar al Assad. Wameshindwa kuelewana juu ya mambo muhimu kama iwapo wanapaswa kufanya mazungumzo na serikali, kuingizwa kwa majeshi ya nje katika mgogoro wa nchi yao, na sera itakayoiongoza nchi baada ya rais Bashar al Assad kuondolewa madarakani. Mgawanyiko wa makundi hayo unaakisi tofauti zilizopo katika jamii ya Syria yenye tofauti za kimawazo, kikabila na umri.

Hata hivyo, kikundi kikubwa kinachopigana na serikali ya Syria, Jeshi huru la Syria, hakihudhurii mkutano huo, kwa madai kwamba mkutano huo ni wa kisiasa, na hivyo hauwahusu waasi.

Akizungumza juu ya mkutano huo wa Cairo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema kuwa ni muhimu kwa makundi ya Syria kuungana na kuwa na mshikamano, na kuwa na uwakilishi mmoja. Mkutano huo unafanyika huku juhudi za nchi za magharibi kumtimua madarakani rais Bashar al Assad zikionekana kugonga mwamba.

Assad asikitishwa na kuangushwa kwa ndege ya Uturuki

Kudunguliwa kwa ndege ya Uturuki kulikofanywa Syria kulizidisha mvutano kati ya nchi hizo
Kudunguliwa kwa ndege ya Uturuki kulikofanywa Syria kulizidisha mvutano kati ya nchi hizoPicha: REUTERS

Wakati hayo yakiarifiwa, gazeti moja la nchini Uturuki limemnukuu Rais Bashar al Assad akisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha jeshi lake kuidungua ndege ya kivita ya Uturuki. Hata hivyo, Assad hakuomba radhi kwa kitendo hicho, akisema ndege hiyo ilikuwa imeingia katika anga ya Syria bila kibali, na ilipitia sehemu ambayo ilitumiwa na ndege za Israel kufanya mashambulizi dhidi ya jengo moja ndani ya Syria mwaka 2007. Rais Assad amesema hataki vita kati ya nchi yake na Uturuki.

Kwa mujibu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake nchini Uingereza, watu 16,500 wamekwisha uawa tangu mgogoro wa Syria ulipoanza. Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, limesema leo kuwa serikali ya Syria imefanya unyanyasaji wa raia ambao unaweza kuchukuliwa kama uhalifu dhidi ya binadamu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE/DPA

Mhariri:Miraji Othman