Wanasiasa watajwa katika kashifa ya "Paradise Papers"
6 Novemba 2017Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung lililofanikiwa kupata taarifa za nyaraka hizo zilizofichuliwa, waandishi wa habari wapatao 400 kutoka nchi 67 waliokuwa wakifuatilia uchunguzi wa suala hilo wamefanikiwa kufichua nyaraka za siri milioni 13.4 ambapo pia waliweza kufichua mbinu zinazotumiwa na matajiri wakubwa pamoja na wanasiasa wa ngazi za juu katika kukwepa kodi. Nyaraka hizo zilizopewa jina la "Paradise Papers" zinaaanzia kipindi cha mwaka 1950 hadi mwaka 2016 zikihusisha barua pepe, mikataba ya kibiashara pamoja na taarifa za kibenki.
Majina ya wanasiasa zaidi ya 120 kutoka karibu mataifa 50 wakiwemo maafisa wa serikali ya rais wa Marekani Donald Trump na makampuni ya Urusi yametajwa katika nyaraka hizo.
Nyaraka hizo zinaonesha pia kuwa kwa kutumia makampuni yasiyofanya biashara, makampuni kama vile Nike, Apple, Uber na Facebook yanaweza kupunguza viwango vyao vya kodi kuwa vya chini zaidi.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung makampuni ya Rock star Bono pamoja na kampuni binafsi ya Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza nayo pia yamehusishwa katika kashifa hiyo. Gabriel Zucman ambaye ni mchumi amelieleza gazeti la Suddeutsche Zeitung kuwa wanasiasa pamoja na watu hao maarufu ulimwenguni wameficha kiasi cha dola trilioni 9.1 katika akaunti za nje.
Jina la Malkia Elizabeth latajwa katika kashifa ya Paridise
Kuhusina na suala linalomuhusu Malkia Elizabeth kumiliki makampuni binafsi nje ya nchi, wakosoaji wanaweza wakahoji iwapo ni sawa kwa kiongozi mkuu wa nchi kujihusisha kukwepa kodi kupitia makampuni aliyowekeza nje ya nchi.
Taarifa hizo zilizofichuliwa zimechapishwa pia na mashirika kadhaa ya habari kwa kushirikiana na taasisi ya waandishi wa habari inayohusika na habari za uchunguzi yenye makao yake nchini Marekani (ICJ).
Taarifa hizo pia zimemuanika waziri wa masuala ya biashara wa Marekani Wilbur Ross, anayedaiwa kushirikiana na washirika wa karibu wa rais wa Urusi Vladimir Putin akiwemo mkwe wa kiume wa rais huyo.
Katika ripoti yake gazeti la Suddeutsche Zeitung limeandika kuwa " Bilionea Wilbur Ross anatengeneza pesa kutokana na biashara anayofanya na Urusi na kuongeza kuwa licha ya kuwa katika baraza la mawaziri la rais Donald Trump hilo tu halimfanyi ajiondoe katika kashifa hiyo.
Ross anaripotiwa kuwa mmoja wa wanaomiliki kampuni ya usafirishaji mizigo kwa njia ya bahari ijulikanayo kama Navigator ambayo imetumia zaidi ya dola milioni 68 ikilihusisha shirika la masuala ya nishati nchini Urusi tangu mwaka 2014. Aidha gazeti la New York Times limeripoti kuwa sehemu ya utajiri alionao Ross inatokana na mbinu anazotumia kukwepa kodi katika masuala yake ya kibiashara.
Ukimuacha Ross, washauri kadhaa wa rais Donald Trump, mawaziri na wafadhili wakati wa kampeni yake nao pia majina yao yanaonekana katika nyaraka hizo za Paradise zilizofichuliwa na waandishi wa habari za uchunguzi.
Kashifa hii pia imekumbusha ujumbe ulioandikwa katika ukurasa wa twitter na rais Donald Trump Juni 18,2013 wakati aipoandika kuwa shindano la urembo la "Miss Universe" litatangazwa moja kwa moja kutoka mjini Moscow Novemba 9 na kusema ni biashara kubwa itakayozileta nchi hizo mbili pamoja na kuhoji iwapo rais Vladimir Putin angekwenda katika shindano hilo basi angekuwa rafiki yake? Oktoba 17,2013 Trump alikieleza kipindi flani cha charti za muziki kuwa amefanya biashara ya kutosha na warusi.
Taarifa zinazohusiana na nyaraka hizo za Paradise Papers zinaonesha kuwa Kansella wazamani wa Ujerumani Gehard Schrouder alikuwa akiliongoza kampuni moja nje ya nchi. Mwaka 2009 alikuwa sehemu ya bodi huru ya ushauri ya kampuni yenye ubia kati ya Uingereza na Marekani ijulikanayo kama TNK-BP huku fedha za urusi zikiendelea kuingia nchini Ujerumani licha ya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.
Gazeti la Suddeutsche Zeitung nalo pia limewahi kuandika taarifa za kashifa nyingine inayofanana na hiyo ijulikanayo kama Panama Papers.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe
Mhariri : Iddi Ssessanga